Aug 30, 2018 16:30 UTC
  • Kamisheni ya Haki za Binadamu ya UN yamtaka Aung San Suu Kyi ajiuzulu

Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imekemea jinai zinazofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo na uungaji mkono wa kiongozi wa chama tawala Aung Saun Suu Kyi na imemtaka ajiuzulu.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Zaid Raad al Hussein amesema kuwa, badala ya kutetea na kutaka kuhalalisha mauaji na jinai zinazofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya, mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi anapaswa kufikiria suala la kuwekwa tena katika kifungo cha nyumbani. 

Vilevile Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia, Seifuddin Abdullah ametoa taarifa akitaka kutekelezwa haki na uadili dhidi ya watu waliohusika na mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar. 

Miito hiyo imetolewa baada ya Kamati ya Kutafuta Ukweli ya Umoja wa Mataifa kusema katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba, kuna udharura wa kufanyika uchunguzi mkubwa kuhusu majenerali wa ngazi za juu wa jeshi la Myanmar akiwemo mkuu wa jeshi la nchi hiyo, Jenerali Min Aung Hlaing na kuwafungulia mashtaka ya kufanya mauaji ya umati katika jimbo la Rakhine, kufanya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu dhidi ya Waislamu wa Rohingya katika majimbo mbalimbali ya nchi hiyo. 

Ripoti iliyotolewa na kamati hiyo imeongeza kuwa, jeshi la Myanmar limefanya jinai kubwa dhidi ya binadamu ikiwa ni pamoja na kuua, kunajisi, kutesa, kuwafanya watu kuwa watumwa, ukatili dhidi ya watoto na kuharibu kabisa vijiji vya Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Wasichana wa Kiislamu wa jamii ya Rohingya wanabakwa na kujajisiwa.

Hata hivyo Aung San Suu Kyi ambaye ni Mshauri Mkuu wa Serikali ya Myanmar na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo amepinga wito wa kamati hiyo ya Umoja wa Mataifa wa kufikishwa mahakamani majenerali hao wa jeshi waliofanya jinai za kivita na mauaji ya kimbari.

Mauaji ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar yalianza katika muongo wa 1960 na yameshadidi katika mwaka mmoja uliopita chini ya kivuli cha kimya cha jamii ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa na Baraza lake la Usalama. Katika kipindi hicho chote maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wameuawa, kunajisiwa, kufanywa watumwa na mamilioni ya wengine wamelazimishwa kukimbia makazi na nchi yao. Jinai na uhalifu huo unaofanyika kwa mpangilio maalumu bado unaendelea mbele ya macho ya madola makubwa ya Magharibi yanayodai kuwa yanatetea demokrasia ya haki za binadamu duniani.

Mtaalamu wa masuala ya kisiasa ya kimataifa, Fransis Vid anasema: "Waislamu wa jamii ya Rohingya huko Myanmar wanaendelea kuuawa na jeshi la nchi hiyo na duru za kimataifa zilikuwa na matarajio kwamba, San Suu Kyi ambaye yeye mwenyewe alionja machungu ya mashinikizo mbalimbali, angechukua hatua ya kimsingi ya kukomesha uhalifu na mauaji ya raia hao wasio na hatia nchini kwake."

San Suu Kyi anatetea mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Rohingya.

Duru za kisiasa zinaamini kuwa, ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Kamati ya Kutafuta Ukweli ya Umoja wa Mataifa ambayo imewatambua majenerali wa jeshi la Myanmar kuwa wamehusika na mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Rohingya ni fursa nzuri kwa umoja huo kuchukua hatua za awali za kuwafikisha mahakamani watenda jinai hao.

Wakati huo huo Mshauri Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Kuzuia Mauaji ya Kimbari, Adama Dieng anasema: "Ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa na jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya unatisha sana. Hakika ripoti iliyotolewa na UN kuhusu mauaji ya Waislamu hao inatia nguvu tuhuma zinazolikabili jeshi na serikali ya Myanmar."

Waislamu wa Myanmar wanahitaji msaada wa jamii ya kimataifa.

Alaa kulli hal, sasa na baada ya kamati ya kutafuta ukweli kuthibitisha kwamba, jeshi la Myanmar limehusika na mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu nchini humo, Umoja wa Mataifa hauna tena kisingizio cha kutowafikisha katika mahakama za kimataifa wahusika wakuu wa uhalifu huo. Kwa msingi huo Waislamu wa Myanmar na wapenda haki kote duniani wanatarajia kwamba, UN itachukua hatua na kutumia ripoti ya Kamati ya Kutafuta Ukweli huko Myanmar kuwafikisha mahakamani watendaji jinai na uhalifu hususan majenerali wa jeshi la Myanmar.   

Tags

Maoni