Aug 31, 2018 03:01 UTC
  • Siasa za Trump, hatari kwa

Mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amekiambia kikao cha Baraza la Usalama kilichokutana kujadili maudhui ya upatanishi na kutatua hitilafu kwamba moja kati ya misingi ya Umoja wa Mataifa ni kwamba dunia ipaswa kuongozwa kwa sheria na si kwa kutumia mabavu.

Gholamali Khoshrou ametoa mfano wa sera za utumiaji mabavu duniani kwa kusema kuwa, Marekani inakiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na inazihamasisha nchi nyingine kuasi azimio hilo na kuzitisha kwamba iwapo hazitafanya hivyo zitakabiliwa na adhabu kali. 

Itakumbukwa kuwa, tarehe 8 Mei mwaka huu wa 2018 Rais Donald Truump wa Marekani alipuuza azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililothibitisha makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA. Baada ya kuchukua hatua hiyo serikali ya Trump pia inatumia njia mbalimbali kuzizuia nchi zilizotia saini makubaliano hayo na nyinginezo zisishirikiane na Iran katika masuala ya uchumi. Katika mkondo huo wawakilishi wa Marekani wamekuwa wakisafiri katika nchi mbalimbali duniani na kuzitisha kwamba, zitakabiliwa na adhabu iwapo zitashirikiana kiuchumi na Iran. Mwenendo huu wa Marekani ni kielelezo cha kutumia "mabavu" katika siasa za kimataifa. Kuendelea kwa siasa kama hizi ni hatari kubwa kwa mfumo unaotawala dunia unaosisitiza udharura wa kushirikiana na kutumia njia za amani kwa ajili ya kutatua masuala mbalimbali ya kimataifa.

Donald Trump

Kujiondoa Marekani katika makubaliano ya kimataifa kama makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni mfano wa wazi wa siasa haribifu za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja. Vilevile kutoa vitisho dhidi ya nchi mbalimbali kwa sababu ya kushirikiana na Iran, vita vya kibiashara dhidi ya Ulaya, China na Russia na kujiondoa Marekani katika mikataba na makubaliano ya kimataifa, yote hayo na mengine ni ishara za sera za utumiaji mabavu za serikali ya Donald Trump. Kwa msingi huo kuna udharura wa jamii ya kimataifa kuchukua msimamo mmoja wa kukabiliana na sera na misimamo kama hiyo ya kukanyaga na kudharau utawala wa sheria. 

Wataalamu wa mambo pia wanasisitiza kuwa, kuendelea kwa mwenendo huu kunashusha hadhi na heshima ya Umoja wa Mataifa na Baraza lake la Usalama na kuielekeza dunia katika machafuko na vita kutokana na kukanyagwa na kupuuzwa "utawala wa sharia".

Msimamo wa jamii ya kimataifa kuhusu sera hizo za Trump unaonesha kuwa, walimwengu hawakubaliani na siasa hizo za kibabe na kibeberu. Dilip Hiro, mwandishi wa Kimarekani na mtaalamu wa masuala ya kimataifa hivi karibuni aliuambia mtandao wa Global Research kwamba: "Katika kipindi hiki cha uongozi wa Donald Trump dunia imetoa ujumbe wa wazi unaosema kuwa, haitakuwa uwanja wa michezo wa Rais wa Marekani.

Mwandishi huyo wa Marekani amesisitiza kuwa: "Siasa za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Trump katika medani ya biashara, kujiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya Iran na makubaliano ya hali ya hewa ya Paris ni mwanzo wa harakati ya kimataifa dhidi ya Trump."

Siasa za kibeberu za Trump zinapingwa na jamii ya kimataifa.

Wakati huo huo mtandao wa Asia Times umekosoa siasa haribifu za serikali ya sasa ya Marekani katika upeo wa kimataifa na kuandika kuwa: "Kwa sasa dunia imekuwa chungu kwa Rais wa Marekani. Siasa za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Trump, vita vya kibiashara na kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia na Iran sambamba na gharama kubwa za ulinzi na vilevile siasa za kimataifa zinazohusiana na kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa, vimezusha wimbi kubwa la malalamiko dhidi ya Trump si katika upewa wa kimataifa pekee, bali hata ndani ya Marekani kwenyewe."

Wimbi hili la upinzani dhidi ya siasa za kibeberu za Marekani ni ishara kwamba, dunia haikubali kuwa punda anayehudumia malengo na maslahi ya Marekani. Hivyo, jambo pekee litakalodhamini na kulinda amani ya kimataifa ni utawala wa sharia na kutumia njia za amani kutatua matatizo ya kimataifa, la sivyo dunia itakabiliwa na mustakbali mweusi utakawaelekeza kubaya walimwengu wote.      

Tags

Maoni