Sep 01, 2018 07:36 UTC
  • Sisitizo la Rais wa Uturuki la kuondolewa sarafu ya Dola katika biashara ya kimataifa

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki amesisitizia umuhimu wa sarafu ya nchi yake kutumika katika mabadilishano ya kibiashara na pia kutumiwa nafasi ya kiuchumi ya nchi zinazozungumza Kituruki.

Rais Erdoğan ameyasema hayo kabla ya kufanya ziara rasmi nchini Kyrgyzstan na kuongeza kwamba: "Ni lazima tuonyeshe ushirikiano athirifu kwa ajili kuhitimisha ubabe wa Dola ya Marekani katika biashara ya kimataifa." Mwisho wa kunukuu. Kadhalika Rais Recep Tayyip Erdoğan ameashiria juu ya udharura wa kunusuriwa uchumi wa nchi tofauti za dunia kutokana na udikteta wa sarafu ya Dola na kutangaza kwamba, Uturuki inaweza kushirikiana na Kyrgyzstan kusonga mbele katika mabadilishano ya kibiashara kwa msingi wa sarafu ya fedha za nchi hizo. Mbali na hayo rais huyo wa Uturuki ameashiria pia nafasi ya kiuchumi ya nchi za Asia na kusema kuwa, katika mkutano wa sita wa Baraza Kuu la Nchi Zinazozungumza Lugha ya Kituruki ambao umepangwa kufanyika nchini Kyrgyzstan, nchi za Uturuki, Kyrgyzstan, Azerbaijan, Turkmenistan, Uzbekistan na Kazakhstan zitajadili suala hilo. Leo Rais Erdoğan, anatazamiwa kuwa mgeni wa Rais Sooronbay Jeenbekov wa Kyrgyzstan.

Sarafu ya Dola ambayo imekuwa ikitumiwa na Marekani katika kuziadhibu nchi mbalimbali duniani

Inaonekana kwamba Uturuki inafanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuzuia ubeberu wa sarafu ya Dola katika mfumo wa mabadilishano ya kibiashara duniani. Uturuki imewekewa vikwazo na Marekani, huku mahusiano yake yanayolegalega na nchi za Magharibi hivi karibuni yakipelekea kuporomoka thamani ya sarafu yake ya kitaifa mkabala wa Dola ya Marekani. Matukio hayo yamekuwa na taathira hasi kwenye uchumi wa serikali ya Ankara. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Uturuki ikapendelea kuunda mfumo ambao utaweza kupunguza thamani ya Dola na kwa kutumia sarafu ya Lira, iweze kupandisha thamani ya sarafu hiyo. Katika uwanja huo, matumizi ya fedha hiyo ya kitaifa katika mabadilishano ya kibiashara, ni njia bora ya kulinda thamani yake. Kilicho na umuhimu katika suala hili ni kwamba, Uturuki inaitazama kadhia hiyo kwa mtazamo mpana zaidi ambapo inataka kuanzisha mfumo maalumu wa kimataifa ambao utazishirikisha pia nchi kubwa tofauti.

Marais wa Marekani na Uturuki ambao kwa sasa wamekuwa mahasimu

Hususan kwa kutilia maanani kwamba, uwepo wa nchi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, China na Russia, ambazo zinafuatilia kujiondoa katika utawala wa mfumo wa Dola, unaweza kusaidia juhudi za Ankara za kusambaratisha udhibiti wa sarafu hiyo ya Marekani. Ukweli ni kwamba, udhibiti wa Dola katika mfumo wa uchumi kimataifa, umeisababishia matatizo mengi jamii ya kimataifa, kiasi cha kuzifanya nchi nyingi kutaka kujitoa katika makucha ya sarafu hiyo ya kibeberu. Katika uwanja huo, Kimberly Amadeo mchambuzi wa masuala ya kisiasa anaandika kwamba: "Udhibiti wa sarafu ya Dola na dunia kupendelea kutumia sarafu moja maalumu katika miamala ya kimataifa, kumeifanya sarafu hiyo kuwa wenzo wa ubabe wa Marekani." Mwisho wa kunukuu. Kwa kuzingatia hilo, tunaweza kusema kuwa, iwapo hatua ya Uturuki ya kutaka kutumika sarafu za kitaifa katika miamala ya kibishara kimataifa, inalotokana na nia njema na sio harakati ya kisiasa tu, inaweza kuwa na umuhimu mkubwa katika kujaribu kuondokana na mfumo wa kiukandamizi wa matumizi ya Dola duniani. Hasa kwa kutilia maanani kuwa, hivi sasa Uturuki ina washirika wakubwa kibiashara kama vile China, Iran, Russia na Umoja wa Ulaya.

Maoni