Sep 02, 2018 02:21 UTC
  • Nipigie baada ya dakika 30: Waziri Mkuu wa Pakistan amtaka Rais wa Ufaransa angojee kwenye laini ya simu

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alitakiwa angojee kwa muda wa nusu saa kuzungumza na Waziri Mkuu wa Pakistan Imran Khan, baada ya kumpigia simu bila taarifa wakati Waziri Mkuu huyo wa Pakistan akiwa kwenye kikao na shakhsia waandamizi wa vyombo vya habari vya nchi hiyo.

Taarifa zilizothibitishwa na duru mbali mbali zimeeleza kuwa hatimaye Waziri Mkuu Khan alipokea simu hiyo aliyopigiwa bila taarifa na Rais Macron wa Ufaransa siku ya Ijumaa wakati akiwa kwenye kikao na maafisa wa vyombo mbalimbali vya habari vya nchini Pakistan.

Wakati kikao hicho kikiwa kinaendelea katika ofisi ya Imran Khan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan Tehmina Janjua alimwomba Waziri Mkuu Khan apokee simu kutoka kwa rais wa Ufaransa lakini kiongozi huyo alimweleza kuwa ametingwa na kazi na kutaka apigiwe simu baada ya dakika 30.

Hamid Miir, mmoja wa maafisa wa vyombo vya habari aliyehudhuria kikao hicho kilichofanyika kwenye ofisi ya Waziri Mkuu wa Pakistan amethibitisha kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter kujiri kwa tukio hilo juzi Ijumaa.

Tags

Maoni