Sep 02, 2018 10:23 UTC
  • Kuuawa kiongozi wa upinzani wa eneo lenye mamlaka ya ndani la Donetsk, Ukraine na athari zake

Kufuatia kuuawa Alexander Zakharchenko, Kiongozi wa Upinzani wa eneo la Donetsk nchini Ukrain, Rais Vladmir Putin wa Russia ametaka kuchukuliwa hatua kali wahusika wa jinai hiyo.

Zakharchenko aliuawa siku ya Ijumaa katika mripuko wa bomu uliotokea katika mgahawa mmoja mjini Donetsk pamoja na Waziri wa Sheria na Mapato wa eneo hilo linalopigania kujitawala. Katika ujumbe wake wa rambirambi alioutoa kufuatia mauaji ya Zakharchenko, Rais Putin amesema, mauaji ya kikatili dhidi ya mwanasiasa huyo ni ushahidi mwingine kwamba wale waliochagua njia ya mauaji, ukatili na vitisho, hawataki utatuzi wa mgogoro huo kwa njia ya amani na kisiasa, wala hawana nia ya kufanya mazungumzo yenye nia njema na wakazi wa eneo la kusini na mashariki mwa Ukraine. Mwaka 2014 Aleksander Zakharchenko akiwa kiongozi wa upinzani, aliongoza malalamiko dhidi ya serikali kuu ya Kiev, mji mkuu wa Ukraine ambapo alitaka kujitenga eneo la Donetsk na nchi hiyo, suala ambalo liliingiza serikali kuu katika vita vikali vya ndani na wapinzani wanaotaka kujitenga. Mapigano hayo ya miaka mitatu, yalimalizika kwa kutiwa saini 'makubaliano ya Minsk' mji mkuu wa Belarus, ingawa utekelezwaji wa makubaliano hayo bado ni kati ya matatizo ya sasa ya Ukraine.

Rais Vladmir Putin wa Russia ambaye ametaka wahusika wa jinai hiyo wakamatwe haraka

Mwezi Februari 2015 Russia ilitiliana saini na Ujerumani na Ufaransa makubaliano ya amani ya Minsk kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro wa Ukraine, hata hivyo makubaliano hayo hayajatekelezwa kikamilifu. Sehemu ya makubaliano hayo, iliilazimisha serikali ya Kiev kuandaa uchaguzi katika eneo la mashariki mwa nchi, hata hivyo serikali ya Ukraine ilisema kuwa, itaruhusu kufanyika uchaguzi huo endapo tu askari wanaoungwa mkono na Russia wataondoka katika eneo hilo. Hii ni katika hali ambayo viongozi wa Russia wameendelea kusisitiza utekelezwaji wa uchaguzi huo. Katika uwanja huo, Dmitry Peskov Msemaji wa Ofisi ya Rais wa Russia amesema: "Kremlin inaamini kwamba, utatuzi wa kadhia ya Ukraine unategemea utekelezwaji wa makubaliano ya Minsk na utekelezwaji huo unaweza kuwa hatua muhimu katika utatuzi wa kadhia ya nchi hiyo." Mwisho wa kunukuu. Maeneo ya mashariki mwa Ukraine yamekuwa uwanja wa mapigano na mauaji tangu mwaka 2014 kiasi kwamba zaidi ya watu elfu 10 wamepoteza maisha. 

Machafuko ya Ukraine

Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema: "Kiujumla watu milioni nne na laki nne wameathirika na mgogoro wa kijeshi katika eneo la mashariki mwa Ukraine, na zaidi ya watu milioni moja na nusu wengine wamekuwa wakimbizi katika maeneo ya mashariki na kusini mwa nchi kutokana na ghasia hizo." Mwisho wa kunukuu. Hivi sasa pia mauaji dhidi ya Aleksander Zakharchenko, Kiongozi wa Upinzani wa eneo la Donetsk, yameshadidisha hali ya mambo kiasi cha kuzifanya serikali za Russia na Ukraine kutuhumiana juu ya jinai hiyo. Katika uwanja huo, Maria Zakharova Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema: "Kiev imeshatumia mara nyingi njia hiyo kwa ajili ya kuwamaliza wapinzani wake." Mwisho wa kunukuu. Katika sehemu nyingine ni kwamba mauaji dhidi ya mwanasiasa huyo wa upinzani yametokea katika hali hali ambayo siku chache zilizopita, alitangaza utayarifu wake kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi wa rais wa eneo hilo. Alaakullihal, katika hali ambayo  namna ya kutekelezwa makubaliano ya Minsk na kutafuta njia ya utatuzi wa mapigano ya ndani, inatajwa kuwa changamoto muhimu kwa serikali ya Ukraine na Russia, inaonekana kwamba kuuawa Zakharchenko, kutaufanya mgogoro wa kisiasa kati ya nchi mbili hizo kuwa mkubwa zaidi.

Tags

Maoni