Sep 04, 2018 02:34 UTC
  • Canada yaunga mkono mapatano ya nyuklia ya Iran na kuondoa utegemezi kwa sarafu ya dola ya Marekani

Maamuzi ya upande mmoja ya kisiasa na kimabavu ya Marekani katika kipindi cha utawala wa rais Donald Trump yanaendelea kukabiliwa na upinzani kote duniani.

Kati ya maamuzi hayo ya Trump ni kujiondoa katika mapatano muhimu ya kiuchumi, kuanzisha vita vya kibiashara na washirika pamoja na washindani wa Marekani, kutoa vitisho na hata kuwawekea vikwazo waitifaki wake. Hatua hizo zimepelekea serikali nyingi zichukue hatua za kupunguza athari haribifu za maamuzi ya Marekani yaliyojaa uhasama; na kati ya hatua hizo ni kuundwa mfumo huru wa kifedha usiotegemea sarafu ya dola ya Marekani. Aidha nchi hizo zinalenga kutupilia mbali dola ya Marekani katika mabadilishano ya kibiashara na badala yake kutumia sarafu nyinginezo za kigeni au sarafu zao za taifa.

Hivi karibuni Heiko Maas Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani alizungumzia ulazima wa kuwepo mfumo huru wa kifedha usiotegemea dola ya Marekani ili kukabiliana na mashinikizo ya Washington hasa kuhusiana na mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA. Canada nayo pia imejiunga na kambi mpya inayotaka kutupilia mbali dola ya Marekani.

Kuhusiana na hilo, Chrystia Freeland, Waziri wa Mambo ya Nje wa Canada sambamba na kuunga mkono JCPOA ametangaza pia kuafiki fikra ya kuanzishwa mfumo wa kifedha usiotegemea dola ya Marekani.

Katika mahojiano, Freeland ameunga mkono pendekezo la Ujerumani la kuunda mfumo huru wa kifedha usiotegemea dola ya Marekani na kusema: "Kwa mtazamo wangu, pendekezo hili inapasa lifuatiliwe kwa kina. Fikra hii inatoa matumaini na ina umuhimu zaidi kwa mashirika ya Ulaya kuliko hata yale ya Canada."

Hivi sasa Canada inazozana na Marekani kuhusu Mkataba wa Biashara Huru wa Amerika ya Kaskazini (NAFTA). Trump anakosoa vikali mkataba huo na kuutaja kuwa mbaya na usiofaa kwa Marekani. Mbali na hayo Trump ameongeza ushuru wa forodha  kwa bidhaa za chuma na aluminiamu kutoka Canada, nchi ambayo imekuwa ikihesabiwa kama mshirika wa Marekani katika eneo la Amerika Kaskazini. Hatua hiyo ya Trump imepelekea kuvurugika uhusiano wa nchi hizo mbili.

Katika upande mwingine, hatua ya Trump ya kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran na kuyawekea mashinikizo mashirika na benki za Ulaya ili kuzuia kuwepo mabadilishano ya kifedha na kibenki baina ya Iran na Ulaya ni hatua ambayo imezikasirisha nchi za Ulaya. Kwa kuzingatia nukta hizo, Canada sasa imetangaza kuwa tayari kushirikiana na Ulaya katika kukabiliana na uhasama wa Trump.

Ni wazi kuwa dunia inapinga sera za Trump za kushinikiza mataifa mengine  na hasa sera kuyawekea mataifa mengine vikwazo na kutumia sarafu ya dola kisiasa kushinikiza nchi zingine kiuchumi.

A. Wess Mitchell, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika masuala ya Ulaya na Asia anasema: "Vikwazo ni chombo cha kistratijia na hivi sasa Marekani imeweka vikwazo 4,190 kote duniani na kati ya hivyo kuna vikwazo 580 dhidi ya Russia."

Sera hizo za Marekani za kutumia vikwazo kufikia malengo yake haramu ni jambo ambalo linapingwa na jamii ya kimataifa kiasi kwamba hivi sasa Marekani imeanza kutengwa hatua kwa hatua kote duniani.

Kwa hakika Marekani imetumia vibaya suala la dola yake kuwa sarafu kuu ya kimataifa na imekuwa ikitumia suala hilo kuwashinikiza wengine. Ni kwa sababu hiyo ndio nchi kadhaa sasa zikiwemo zile ambazo ni washirika wa Marekani zikaanzisha mkakati wa kutupilia mbali dola na kutumia sarafu nyinginezo.

Kuendelea mkondo huu kutepalekea kudhoofika dola ya Marekani katika mabadilishano ya kibiashara duniani.

Hakuna shaka kuwa, sera na hatua za Trump zimechangia pakubwa kuanza kutupiliwa mbali sarafu ya dola. Hivi sasa serikali nyingi duniani zimefikia natija kuwa, wakati umewadia kupunguza utegemezi kwa sarafu ya dola ya Marekani.

 

 

Tags

Maoni