Sep 06, 2018 07:19 UTC
  • Dunia yapinga hatua ya Marekani kukata misaada ya shirika la UN linalohudumia wakimbizi wa Palestina

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania amesema nchi yake inalenga kuongeza maradufu misaada yake kwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA) baada ya Marekani kukata misaada yake kwa shirika hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania Josep Borrell ameyasema hayo mbele ya waandishi habari mjini Madrid akiwa ameandamana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya  Palestina Riyadh al-Maliki. Borrel amesisitiza kuwa kutokana na kuwa Marekani sasa inataka sera zake ziendane sawa na za utawala wa Israel, imepoteza ustahiki wa kuwa mpatanishi katika pande mbili za mzozo wa Mashariki ya Kati.

Kauli hiyo ni jibu kwa uamuzi wa Ijumaa iliyopita wa Marekani kukata misaada yake kwa UNRWA. Nchi nyingi duniani zimejiunga na Umoja wa Mataifa katika kulaani hatua hiyo ya upande mmoja ya Marekani.

Aidha taasisi za kimataifa na nchi nyingi duniani zimetangaza kuwa zitaongeza misaada yao kwa UNRWA ili kukabiliana na uamuzi huo hasimu wa Marekani.

Uingereza, Ujerumani na Jordan ni kati ya nchi ambazo zimejiunga na Umoja wa Mataifa kulaani uamuzi huo wa Marekani na ni utawala wa Kizayuni wa Israel pekee ndio uliounga mkono uamuzi huo wa Marekani. Hii ni kwa sababu uamuzi huo ulikuwa ni kwa maslahi ya utawala huo wa Kizayuni na kwa msingi huo Marekani ambayo imekuwa ikidai kuwa ni mpatanishi wa kadhia ya Palestina sasa imeunga mkono kikamilifu upande mmoja katika mgogoro huo wa Mashariki ya Kati. Nukta ya kutaamali hapa ni kuwa, nchi za Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi zikiongozwa na Saudi Arabia zimenyamazia kimya uamuzi huo wa Marekani na ni wazi kuwa yamkini baraza hilo lina mapatano ya siri na utawala wa Kizayuni wa Israel kuhusu jambo hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania Josep Borrell (kulia)  akiwa ameandamana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Mamlaka ya Ndani ya  Palestina Riyadh al-Maliki.

Umoja wa Ulaya pia umesema maamuzi ya upande mmoja ya Marekani yanaleta hasara kwa amani na uthabiti duniani mbali na kuvuruga jitihada za utatuzi wa mgogoro wa Palestina.

Visingizio ambavyo Marekani imetumia katika kukata misaada yake kwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA) vimepingwa vikali na jamii ya kimataifa ambayo inasema visingizio hivyo havina mashiko wala itibari.

Uamuzi kuhusu UNRWA sawa na maamuzi mengine ya utawala wa sasa wa Marekani katika sera za kigeni hayana msingi wowote wa kimantiki wala busara. Kujiondoa Marekani katika mapatano ya nyuklia ya Iran, JCPOA, mapatano ya tabia nchi ya Paris na mapatano mengine muhimu ya kimataifa pamoja na sera zingine zilizotangazwa na utawala wa Trump katika uga wa kimataifa ni mambo ambayo yamepelekea Marekani itambuliwe kama nchi inayovunja ahadi na inayokwepa majukumu yake kimataifa. Sera hizo zimepelekea hata waitifaki wa karibu wa Marekani waingiwe na wasiwasi na walaani vikali hatua za utawala wa Trump.

Rais Trump wa Marekani

John Laughland, mwanafalsafa, mwanahistoria na mwandishi maarufu wa Uingereza anasema uamuzi wa Marekani kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya Iran na maptano ya tabia nchi ya Paris ni hatua ambazo zimeifanya Marekani itambulike kama mshirika asiyeaminika na hilo limewakasirisha waitifake wake barani Ulaya.

Sera za upande mmoja na za kujitakia makuu za Marekani sasa zimepelekea itazamwe na dunia na hasa wiatifaki wake wakuu wa jadi kuwa nchi isiyoweza kuaminika tena. Natija ya hilo ni kuwa hivi sasa Marekani imeanza kutengwa kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa duniani.

Hatua ya Marekani kukata misaada ya UNRWA ni katika fremu ya mpango wa Washington wa kile inachokitaja kuwa  'Muamala wa Karne" katika kadhia ya Palesitna. Hivyo uamuzi huo umechukuliwa kwa lengo la kuwashinikiza zaidi Wapalestina ili wasalimu amri na waache kupigania ukombozi wa ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu na Israel. Kwa kuzingatia mshikamano wa dunia katika kuwasaidia Wapalestina na kutengwa Marekani, itakuwa vigumu kwa Washington kufikia malengo iliyoyakusudia katika kukata misaada yake kwa UNRWA.

Tags

Maoni