Sep 08, 2018 01:24 UTC
  • Kuongezeka mivutano baina ya Russia na Magharibi kuhusu tukio la Salisbury

Kuzushwa upya madai ya kupewa sumu ya kemikali, jasusi Wa zamani wa Russia, Sergei Skripal, na binti yake katika mji wa Salisbury, wa kusini mwa Uingereza mwezi Machi 2018, kumezua mzozo na mivutano mikubwa baina ya nchi za Magharibi na Russia.

Serikali ya Uingereza inadai kuwa Moscow ndiyo iliyompa sumu jasusi huyo na binti yake kwani gesi ya sumu ya Novichok  iliyotumika imetengenezwa Russia na London ikatumia kisingizio hicho kuwafukuza nchini humo wanadiplomasia 23 wa Russia. Hata hivyo serikali ya Moscow imekanusha vikali madai hayo na kusema kwamba, kwanza hakuna uthibitisho wowote kuwa jasusi huyo amepewa sumu, pili inahoji kwa nini London ilikataa ombi la Moscow la kumuonesha hadharani jasusi huyo kuthibitisha kweli amepewa sumu. Kwa upande wake, Russia nayo iliwafukuza makumi ya wanadiplomasia wa Uingereza kulipiza kisasi cha hatua kama hiyo iliyochukuliwa na London dhidi ya wanadiplomasia wake. 

Waziri Mkuu wa Britania, Theresa May, bungeni

 

Hata hivyo kadhia ya Salisbury sasa imechukuua mkondo mpya. Theresa May, waziri mkuu wa Uingereza siku ya Jumatano na baada ya kupita miezi sita tangu kutolewa madai ya kutokea tukio hilo, alisema bungeni kuwa uchunguzi wa mashirika ya kijasusi ya Uingereza umegundua kuwa, maafisa wawili wa kijasusi wa jeshi la Russia walihusika katika tukio hilo. Baada ya hapo waziri mkuu wa Uingereza ameitaka Russia iikabidhi London watu hao wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo, suala ambalo limeungwa mkono pia na nchi nyingine za Magharibi. Viongozi wa nchi nne za Ujerumaini, Ufaransa, Canada na Marekani wametoa tamko la pamoja la kuunga mkono ripoti ya kijasusi ya Uingereza kuhusu tukio hilo na kudai kwamba viongozi wa ngazi za juu wa Russia walikuwa na habari kuhusu operesheni ya kupewa sumu jasusi Skripal na binti yake. Viongozi hao wametoa matamshi makali ya kuonesha hasira zao kuhusu kutumika gesi ya sumu ya Novichok kumshambulia jasusi huyo wa zamani wa Russia. Hata hivyo hatua ya nchi hizo nne za Magharibi imeikasirisha sana Moscow. Vasily Nebenzya, mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa ameitaja London kuwa ni kidhabu katika madai yake hayo na kuongeza kuwa London inafanya njama za kueneza chuki dhidi ya Russia

Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kwa kuzingatia kwamba hivi sasa Uingereza imekaribia kujitoa rasmi katika Umoja wa Ulaya, waziri mkuu wa nchi hiyoi Theresa May anatumia madai hayo kupotosha fikra za walio wengi. Mtaalamu wa masuala ya kimataifa kutoka Russia, Dmitry Igorchenkov anasema, madai ya kupewa sumu jasusi Skripal ni njama za kutaka kupanua wigo wa jeshi la nchi za Magharibi NATO na kuzidi kuiwekea vikwazo Russia kwani Washington na nchi za Ulaya ziko mstari wa mbele wa vita vya kupokezana dhidi ya Russia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov

 

Mgogoro wa kisiasa baina ya Russia na nchi za Magharibi umeingia katika kipindi nyeti na kigumu kutokana na hatua za kulipiziana kisasi zinazochukuliwa na pande mbili. Inaonekana kuwa hivi sasa ni zamu ya Britania kuendesha vita vya nchi za Magharibi dhidi ya Russia kwa uratibu kamili wa viongozi wa nchi za bara hilo. Sergey Lavrov, waziri wa mambo ya nje wa Russia hivi karibuni alisema kuwa, serikali ya Britania imeamua kuchukua hatua za makusudi za kuharibu uhusiano wa Russia na nchi nyingine.

Wakati huo huo nchi za Magharibi zinaonesha wazi kuwa zimeazimia kuendesha vita vikubwa vya kisiasa, kidiplomasia na kipropaganda dhidi ya Russia kwa kutumia madai ya kupewa sumu jasusi wa zamani wa Russia, Sergei Skripal na binti yake huko Salisbury, kusini mwa Uingereza. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa hatua ya serikali ya Russia ya kuisaidia serikali ya Syria kuwaangamiza magaidi waliokuwa wanaungwa mkono na Magharibi na vibaraka wao, imechangia kuongezeka hamaki za nchi hizo na ndio maana zimeamua kuiwekea mashinikizo ya kila upande Russia.

Tags

Maoni