Sep 09, 2018 07:30 UTC
  • Mazungumzo ya Waziri wa Ulinzi wa Iran nchini China na sisitizo la ushirikiano zaidi wa kijeshi na kiuchumi

Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Brigedia Jenerali Amir Hatami ametembelea China kufuatia mwaliko wa waziri mwenzake wa nchi hiyo kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kijeshi na kiuchumi baina ya China na Iran.

Akiwa mjini Beijing amefanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi wa China Luteni Jenerali  Wei Fenghe kuhusu maudhui za kieneo na ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi baina ya nchi mbili.

Mawaziri wa ulinzi wa Iran na China katika mazungumzo yao wamejadili ulazima wa kuwepo ushirikiano katika masuala ya eneo hasa kutokana na hatua ya Marekani ya kuendelea kuibua migogoro Kusini Magharibi na Magharibi mwa Asia.

Aidha Waziri wa Ulinzi wa Iran alikutana na Zhang Youxia Naibu Mkuu wa Tume Kuu ya Kijeshi ya China na huku akiashiria hali nyeti hivi sasa duniani hasa eneo la Asia Magharibi, amesema ushirikiano wa Iran na China katika kuleta amani, uthabiti na usalama ni wa dharura.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo unaohitajika wa kujihami na kukabiliana na vitisho lakini pamoja na hayo inafuatilia malengo mawili muhimu katika uga wa kijeshi.

Kwanza; Kuinua uwezo wa kujihami katika sekta zinazohitajika hasa katika sekta ya makombora ya kujihami. Suala hili lina umuhimu wa kistratijia katika maudhui ya uwezo wa kujihami na kuzuia hujuma ya adui.

Pili; Kutumia uwezo wa ushirikiano wa kijeshi na nchi zenye misimamo huru ili kuboresha uwezo wa kujihami.

Katika fremu hii, mchakato wa kuendelea kuimarisha uhusiano baina ya Iran na China ni nukta inayoashiria kuwa pande mbili zimechukua hatua za ushirikiano katika masuala ya kieneo na kimataifa.

Mazungumzo ya mawaziri wa ulinzi wa Iran na China mjini Beijing

Sayyid Hadi Afqahi, mtaalamu wa masuala ya Asia Magharibi ambaye pia aliwahi kuwa mwanadiplomasia wa Iran anasema: "Ushirikiano kama huu unaweza kupeleka mbele zaidi ushirikiano wa kijeshi na hata unaweza kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.

Suala hilo linapata muhimu zaidi kutokana na kuwa sehemu kubwa ya uhusiano wa sasa wa China na Iran uko katika uga wa uchumi. Kwa hivyo ushirikiano wa kiusalama baina ya nchi mbili ni nukta ambayo inaweza kutoa dhamana katika uhusiano wa kiuchumi.

Katika upande mwingine uwezo wa kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo unatumika kwa ajli ya kuleta uthabiti na usalama na kukabiliana na ugaidi hasa kundi la ISIS. Nutka hiyo imepelekea kuingia katika duru mpya uhusiano wa Tehran na Beijing. Hivi sasa pande mbili zina azma ya kusogeza mbele zaidi stratijia ya pamoja katika uga wa kijeshi na ushirikiano huu ni nukta ya nguvu katika uhusiano wa nchi mbili.

Hayo yanajiri katika hali ambayo sera za utumiaji mabavu na maamuzi ya upande mmoja ya Marekani katika eneo ni mambo ambayo yamepelekea kukosekana uthabiti na usalama na hivyo kutoa pigo kwa maslahi na ushirikiano wa pamoja katika eneo.

Ni miaka kadhaa sasa tokea makundi ya kigaidi yaibue changamoto kubwa katika usalama wa nusu ya eneo la Asia Magharibi. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikifuatilia amani na usalama duniani na huo ni msingi wa sera yake ya kistratijia. Kwa kuzingatia hilo, Iran imekuwa mhusika muhimu katika mchakato wa kutafuta usalama na amani duniani na hasa katika eneo. Sera hiyo ya Iran ni muhimu kwa China ambayo ni miongoni mwa nchi zenye uchumi mkubwa zaidi duniani. Uthabiti na usalama ni sharti la kuwepo uchumi bora. Hii ni kwa sababu iwapo usalama na uthabiti utakosekana, hakuwezi kuwepo mazingira mazuri ya kustawisha ushirikiano wa kiuchumi. Huo ndio msingi wa safari ya Waziri wa Ulinzi wa Iran nchini China na mazungumzo yake na maafisa wa ngazi za juu wa kijeshi nchini humo.

Tags

Maoni