Sep 12, 2018 01:19 UTC
  • Radiamali ya mahakama ya ICC kwa vitisho vya Marekani

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) yenye makao yake mjini Hague Uholanzi imejibu vitisho vya Marekani kwa kusema kuwa itaendelea kufanya uchunguzi wake kuhusu jinai za kivita zilizofanywa na Marekani nchini Afghanistan.

Mahakama hiyo jana Jumanne ilijibu vitisho vya John Bolton Mshauri wa Usalama wa Taifa wa ikulu ya Marekani (White House) na kueleza kuwa mahakama hiyo itaendelea na uchunguzi wake kuhusu jinai za kivita za Marekani huko Afghanistan licha ya vitisho vya Washington kwamba itawawekea vikwazo majaji na wakaguzi wa ICC.  

John Bolton, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa White House 

Taarifa ya mahakama ya ICC imeongeza kuwa: Mahakama hiyo itaendelea kufanya kazi zake kwa mujibu wa taratibu na mamlaka ya kisheria  bila ya woga wala vitisho vyovyote. John Bolton Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani Jumatatu wiki hii alisema kuwa iwapo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) itaendelea kuchunguza tuhuma za jinai za kivita zinazowakabili wanajeshi wa Marekani katika vita huko Afghanistan; Washington itajibu hatua hiyo kwa kuweka vikwazo. Nyaraka na ushahidi ilionao mahakama hiyo ya ICC unaonyesha kuwa Marekani ulitenda jinai chungu nzima kukiwemo kuua raia, kushambulia maeneo ya raia, vituo vya tiba, shule, misikiti na kuwafunga jela raia wa kawaida tangu ilipovamiwa kijeshi Afghanistan mwaka 2001. 

 

Tags

Maoni