Sep 12, 2018 03:42 UTC
  • Ujumbe wa bunge la Ujerumani: Maafa ya Myanmar ni maangamizi ya kizazi

Ujumbe wa wabunge wa Ujerumani walioitembelea Myanmar wameeleza kuwa jinai zililizofanywa dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini humo si chini ya maangamizi ya kizazi.

Katrin Goring-Eckardt na Renate Kunast wanasiasa kutoka chama cha kijani cha Ujerumani wameashiria safari yao ya karibuni katika mkoa uliokumbwa na machafuko wa Rakhine magharibi mwa Myanmar na kueleza kuwa hatima ya mamia ya maelfu ya Waislamu wa Rohingya katika mkoa huo haijulikani na kwamba mapigano ya kikabila yangali yanaendelea dhidi ya jamii hiyo. 

Waislamu wa Rohingya wakikabiliana na masaibu chungu nzima njiani wakikimbia mashambulizi ya jeshi na Mabudha huko Myanmar

Wanasiasa hao wa chama cha Kijani cha nchini Ujerumani wameongeza kuwa serikali ya kijeshi ya Myanmar imeitenga jamii hiyo ya wachache ya Waislamu wa kabila la Rohingya na kuwanyima haki zao za kiraia; kwa kadiri kwamba hii leo Waislamu hao wanatambulika kama jamii kubwa zaidi ya kabila la waliowachache duniani isiyo na nchi yao ya asili. 

Waislamu wa Rohingya zaidi ya elfu sita wameuawa, elfu nane wamejeruhiwa na wengine karibu ya milioni moja wamekimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh tangu Agosti 25 mwaka jana wakati jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali wa Myanmar walipoanzisha mashambulizi dhidi ya jamii hiyo ya wachache katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi hiyo. Umoja wa Mataifa pia umezitaja jinai hizo dhidi ya Waislamu wa Rohingya huko Myanmar kuwa ni maangamizi ya kizazi. 

Tags

Maoni