Sep 12, 2018 07:11 UTC
  • Umoja wa Ulaya waiunga mkono mahakama ya ICC kuhusiana na Marekani

Umoja wa Ulaya umetoa radiamali yake kwa vitisho vya Marekani vya kutaka kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na kuunga mkono hatua zinazochukuliwa na mahakama hiyo.

Umoja wa Ulaya umetangaza kuwa wahanga wa jinai za kimataifa popote itakapokuwa wanastahiki uadilifu na watenda jinai popote watakapopatikana wanapasa kufikishwa mahakamani na kukuhukumiwa. 

Umoja wa Ulaya umesisitiza kuwa unaendelea kuunga mkono nafasi ya kisheria na jitihada za kufanikisha uadilifu dhidi ya jinai nzito zaidi. Imesema kuwa itaendelea kuiheshimu mahakama ya ICC na shughuli zake. Marekani Jumatatu wiki hii ilichukua uamuzi wa kuishambulia kwa maneno Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) yenye makao yake mjini The Hague Uholanzi na kutishia kuwawekea vikwazo majaji wa mahakama hiyo iwapo wataanzisha uchunguzi kuhusu jinai za kivita za Marekani nchini Afghanistan.  

Mahakama ya ICC jana pia ilitoa jibu kwa vitisho hivyo vya John Bolton Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani vya kutaka kuiwekea vikwazo mahakama hiyo kwa kusema itaendelea kutekeleza majukumu yake bila ya woga wala wasiwasi wowote. 

John Bolton, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa White House 

Nyaraka na ushahidi ilionao mahakama hiyo ya ICC unaonyesha kuwa Marekani ilitenda jinai chungu nzima kukiwemo kuua raia, kushambulia maeneo ya raia, vituo vya tiba, shule, misikiti na kuwafunga jela raia wa kawaida tangu ilipovamiwa kijeshi Afghanistan mwaka 2001. 

Tags

Maoni