Sep 12, 2018 13:25 UTC
  • Radiamali ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC dhidi ya vitisho vya Marekani

Siku moja baada ya John Bolton, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani kutoa matamshi ya vitisho kwamba nchi hiyo itaiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, iwapo itaanzisha uchunguzi kuhusu jinai zilizofanywa na nchi hiyo huko Afghanistan na vilevile zillizofanywa na utawala haramu wa Israel huko Palestina, mahakama hiyo imesisitiza kwamba itaendelea na uchunguzi huo bila ya woga wala kukubali kutishwa.

Mahakam ya ICC iliyo na makao makuu yake mjini The Hague Uholanzi imesisitiza kwamba itaendelea na uchunguzi wake huo bila ya woga wala kusita na kwamba itafanya uchunguzi huo kwa msingi wa sheria zinazotambuliwa kimataifa. Msimamo huo umetangazwa na mahakama ya ICC katika hali ambayo Umoja wa Ulaya pia imeiunga mkono na kuitaka itekeleze shughuli zake bila ya kuingiliwa na mtu wala nchi yoyote. Umoja wa Ulaya unasisitiza kwamba wahanga wa jinai za kimataifa, popote pale walipo, wana haki ya kufanyiwa uadilifu na kwamba wahalifu wa jinai za kivita popote pale walipo, wanapaswa kusimamishwa kuzimbani, kuhukumiwa na kuadhibiwa vilivyo. John Bolton amekosoa na kutishia kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC katika hali ambayo nyaraka za kuaminika ambazo ziko mikononi mwa mahakama hiyo zinathibitisha wazi kwamba tokea Marekani ishambulie na kuikalia kwa mabavu Afghanistan hapo mwaka 2001 hadi sasa, nchi hiyo ya Magharibi imetekeleza jinai nyingi na za kutisha zikiwemo za mauaji ya umati dhidi ya raia, mashambulio katika maeneo ya makazi, vituo vya afya na tiba, shule, misikiti na kuwafunga jela raia kiholela. 

John Bolton, Mshauri wa Masuala ya Usalama wa Taifa wa Marekani

Marekani inatishia kuiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Jinai katika hali ambayo nchi hiyo yenyewe imekuwa ikikiuka waziwazi au kutangaza rasmi kujitoa katika taasisi na mikataba muhimu ya kimataifa. Kwa kutumia nara ya 'Marekani Kwanza' na kwa kisingizio cha kulinda maslahi ya nchi hiyo, Rais Donald Trump ameiondoa nchi hiyo katika mikataba muhimu ya kimataifa ikiwemo ya tabianchi ya Paris, mapatano ya nyuklia ya Iran JCPOA na pia taasisi muhimu kama Baraza la Haki za Binadamu na Shirika la Elimu, Sayanzi na Utamaduni UNESCO, yote mawili yakiwa ni ya Umoja wa Mataifa. Akikosoa vikali msimao wa Marekani kuhusiana na suala hilo, Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amesema kuwa kwa kujitoa katika mikataba muhimu ya kimataifa, rais wa Marekani amepuuza msingi muhimu wa kuheshimiwa mitazamo ya pande kadhaa, na kuamua kufuata mtazamo wa upande mmoja tu katika upeo wa kimataifa. Watawala wa Washigton wanadhani kwamba kwa hatua zao hizo wataweza kuongeza nguvu za Marekani duniani na kudhoofisha mikataba na taasisi za kimataifa. Jambo hilo linathibitishwa wazi na matamshi ya kejeli yaliyotolewa hivi karibuni na  John Bolton kuhusiana na ICC aliposema kuwa Marekani itaiacha mahakama hiyo ikufe.

Makao makuu ya ICC mjini The Hague Uholanzi

Wanachokisahau watawala hao ni kuwa msimamo wao huo hautakuwa na natija nyingine ghairi ya kuwafanywa watengwe zaidi katika ngazi za kimataifa, kama inavyoonekana wazi hivi sasa ambapo washirika wakubwa wa Marekani barani Ulaya wametangaza wazi kwamba wataendelea kuheshimu na kutekeleza mikataba ya kimataifa kama JCPOA na Mkataba wa Tabianchi wa Paris. Wajuzi wengi wa mambo kimataifa wanaamini kwamba msimamo huo wa Marekani pia utachochea kuwepo migawanyiko kati ya mataifa ulimwengunim na hivyo kuongeza uwezekano wa kutokea vita baina yao. Males Hanyg, mwanaharakati wa kisiasa wa Marekani anasema kuhusu suala hilo kwamba siasa hizo za White House zimepelekea kutengwa zaidi Marekani na kuongeza kuwa mitazamo ya upade mmoja ya Trump ni tishio kubwa kwa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimatifa, na kwamba ni chancho cha kuenea vita na ukiukwaji wa haki za binadamu duniani.

Makao Makuu ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, mjini Geneva

Siasa hizo mbovu zinatekelezwa na Marekani katika hali ambayo hivi sasa utandawazi unaendelea kuimarika katika pande zote za dunia ambapo changamoto zilizopo pia zinachukua mkondo huo wa utandawazi. Kwa msingi huo ni wazi kuwa iwapo hakutakuwepo na mtazamo wa kimataifa kuhusu changamoto hizo, itakuwa vigumu kukabiliana nazo. Kuhusu suala hilo, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anasisitiza juu ya kuwepo mtazamo wa kimataifa katika kujaribu kutatua changamoto hizo na kusema, na tunanukuu: 'Watu wanaodhani kwamba leo ni washindi  kesho huenda wakashindwa.' Mwisho wa kunukuu.

Tags

Maoni