Sep 12, 2018 13:55 UTC
  • Junker: Ushirikiano mpya wa AU na EU kubuni nafasi milioni 10 za ajira

Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya amesema EU inapania kuzindua ushirikiano mpya kati yake na Umoja wa Afrika utakaosababisha kubuniwa mamilioni ya nafasi za ajira.

Katika hotuba yake ya kila mwaka katika Bunge la Umoja wa Ulaya hii leo, Jean-Claude Juncker amesema umoja huo unaandaa fremu ya kuvutia uwekezaji mkubwa barani Afrika.

Amesema, "Hii leo, tunapendekeza kuundwa muungano mpya, utakaohakikisha kuwa kuna mchakato endelevu wa kustawishwa uwekezaji na kubuniwa nafasi za ajira baina ya Afrika na Ulaya, mkakati ambao utapelekea kuundwa nafasi milioni 10 za ajira barani Afrika katika kipindi cha miaka mitano ijayo pekee." 

Amebainisha kuwa, "Afrika haihitaji tena misaada, bali inahitaji ushirikiano wa kweli na uadilifu, na sisi Ulaya tunahitaji mshirika wa namna hii pia."

Wahajiri wa Kiafrika wanaohatarisha maisha kwenda kusaka ajira Ulaya

Amesema katika siku zijazo, makubaliano ya kibiashara kati ya nchi za Afrika na Ulaya yatabadilishwa na kuwa makubaliano ya kibiashara ya mabara mawili.

Umoja wa Ulaya umekuwa ukisisitiza kuwa, unajiandaa kubadilisha mkondo na mtazamo wake kwa bara Afrika, na kwamba badala ya kuwa mtoaji misaada kwa nchi za Afrika, uwe mshirikia wake wa kibiashara, kwa shabaha ya kuzuia vijana wa Kiafrika kujiunga na magenge yenye misimamo mikali sambamba na kudhiti wimbi la wahajiri wa Kiafrika wanaokimbilia Ulaya kutafuta ajira.

Tags

Maoni