Sep 17, 2018 07:36 UTC
  • Marekani yamtimua balozi wa Palestina kutoka Washington

Baada ya serikali ya Marekani kukata misaada yake kwa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina la Umoja wa Mataifa (UNRWA), imemtimua balozi wa Palestina kutoka mjini Washington.

Dr. Husam Zomlot, balozi wa Palestina nchini Marekani ameieleza kanali ya televisheni ya al-Mayaadin ya Lebanon kwamba, viongozi wa Marekani wameitaka familia yake kuondoka haraka mjini Washington. Zamlot ameongeza kwamba, viongozi wa Marekani pia wamebatilisha vibali vyao vya kuishi nchi hiyo sambamba na kuwafungia akaunti zao za benki.

Rais Donald Trump wa Marekani anayejaribu kuwashinikiza Wapalestina wakubali mpango wake wa Muamala wa Karne

Tarehe 10 mwezi huu, serikali ya Rais Donald Trump wa Marekani ilitangaza rasmi kufunga ofisi za kidiplomasia za Palestina mjini Washington. Wakati huo huo, ofisi ya uwakilishi ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO mjini Washington ambayo Trump alitoa amri mapema ya kufungwa kwake, ilisimamisha shughuli zake tarehe 13 ya mwezi huu. Hatua hizo ni sehemu ya siasa za serikali ya Trump kwa ajili ya kuwashinikiza Wapalestina waweze kukubaliana na mpango wake wa 'Muamala wa Karne' ambao hadi sasa unaendelea kufeli kutokana na msimamo wa Wapalestina.

Tags

Maoni