Sep 18, 2018 04:38 UTC
  • Trump atoa amri ya kuzipandishia tena ushuru bidhaa za China za thamani ya Dola bilioni 200

Rais Donald Trump wa Marekani amezipandishia ushuru wa asilimia 10 bidhaa za China zinazoingizwa nchi hiyo, ambazo zinakadiriwa kuwa za thamani ya Dola bilioni 200.

Taarifa iliyotolewa na ikulu ya Marekani White House imesema kuwa, Trump ametoa amri hiyo ya ongezeko la ushuru wa forodha wa asilimia 10 kwa bidhaa za China zinazoingizwa Marekani na kwamba amri hiyo itaanza kutekelezwa kuanzia tarehe 24 ya mwezi huu. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, iwapo serikali ya China itachukua hatua ya ulipizaji kisasi kuhusu sekta ya kilimo au ya viwanda ya Marekani, basi Washington itazipandishia tena ushuru bidhaa za China, wa Dola bilioni 267.

Vita vya kibiashara kati ya China na Marekani vinazidi kuongezeka

Trump anadai kwamba ameipatia Beijing fursa iweze kurekebisha mienendo yake kuhusu Marekani, lakini kwamba hadi sasa Beijing haijafanya lolote kuhusu jambo hilo. Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari nchini Marekani, ongezeko hilo jipya la ushuru linazihusu bidhaa elfu sita za China ambapo kwa mara ya kwanza, vifaa vya ndani ya nyumba, mikoba ya mkononi, mashine za kufagia, vifaa vya ujenzi na vyakula vya baharini vimejumuishwa. Awali Marekani na China zilipandishiana ushuru wa Dola bilioni 50 kwa bidhaa zao. Aidha Beijing tayari imetangaza kuchukua hatua ya ulipizaji kisasi kutokana na ushuru huo mpya wa Marekani dhidi yake.

Tags

Maoni