Sep 19, 2018 04:04 UTC
  • Mkutano wa Vienna na uenezaji uongo wa viongozi wa Saudi Arabia

Viongozi wa Saudi Arabia wamekuwa wakitumia kila fursa ili kupotosha mambo na kufunika siasa za uzushaji fitna za utawala wa Aal-Saud.

Mara hii Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia akihutubia katika mkutano wa 62 wa Baraza Kuu la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) mjini Vienna Austria amelitumia vibaya jukwaa la mkutano huo na kudai kwamba, Riyadh inataka 'eneo lisilo na silaha za atomiki' katika Mashariki ya Kati (Magharibi mwa Asia).

Katika hali ambayo, Yukiya Amano, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) alisisitiza mwanzoni mwa mkutano huo kwamba, Iran imefungamana kikamilifu na kutekeleza ahadi zake zote kuhusiana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Khalid  Al-Falih, Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia  alikariri tena madai dhidi ya Iran na kueleza kwamba, Tehran ina miradi ya nyuklia ambayo ya kutiliwa shaka.

Khalid  Al-Falih, Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia

Kwa hakika viongozi wa Riyadh wanafahamu vyema kwamba, tishio la kweli kwa eneo la Mashariki ya Kati linatokana na kukataa utawala haramu wa Israel kujiunga na Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) na kutokubali ombi lolote lile la kufanyika ukaguzi wa kimataifa kwa vituo vyake vya nyuklia. Hata hivyo, viongozi wa Saudi Arabia licha ya kufahamu vyema hilo lakini wanafadhalisha masuala hayo pamoja na uhusiano wao na Tel Aviv visifichuliwe na kufumbia macho ukweli wa mambo.

Mwezi Novemba mwaka jana, Yuval Steinitz Waziri wa Nishati wa utawala ghasibu wa Israel kwa mara ya kwanza alifichua uhusiano wa siri wa utawala huo na Saudi Arabia. Shirikak la Habari la Reuters lilimnukuu Yuval Steinitz akisema: Sisi na Saudi Arabia pamoja na baadhi ya nchi za Kiarabu tuna uhusiano wa kiwango cha siri, na katika hali ya kawaida sio sisi ambao tunaona aibu au kufedheheka kutokana na na kuweko uhusiano huu.

Yuval Steinitz Waziri wa Nishati wa utawala ghasibu wa Israel

Kabla ya hapo pia, Gadi Eizenkot, mkuu wa majeshi ya Israel alisema katika mahojiano yake na gazeti la Saudi Arabia la Elaph kwamba: Iran ndio tishio kubwa zaidi kwa eneo la Mashariki ya Kati na kubainisha kwamba, Tel Aviv iko tayari kubadilishana taarifa na Riyadh kwa shabaha ya kukabiliana na ushawishi wa Tehran katika eneo. Abdolreza Farajirad, balozi wa zamani wa Iran nchini Norway na Hungary, mtaalamu wa masuala ya kimataifa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu anaamini kuwa, uhusiano wa Israel na Saudi Arabia ni mpango ulioandaliwa.

Aidha anasema: Wasaudia wanataka kumridhisha Trump, Marekani na lobi za Kizayuni nchini Marekani. Ndio maana Saudi Arabia inafanya harakati ili ubaya wa kuwa na uhusiano na Tel Aviv uondoke na kwa msingi huo iweze kufuatilia vizuri na bila wasiwasi wowote mipango yake kwa ushirikiano na Marekani na madola ya Magharibi.

Ukweli wa mambo ni kuwa, Saudi Arabia inafanya njama ili haiba na sura yake iliyojaa hadaa ionekane katika asasi za kimataifa kuwa ni chanya, nzuri na yenye kutengeneza mambo na wakati huo huo, iwaonyeshe walimwengu kwamba, Iran ni taifa linalopaswa kuchukiwa. Kukaririwa madai kama hayo yaliyotolewa na Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia bila shaka ni mambo na mipango iliyoratibiwa. Hata hivyo ukweli wa mambo ni kuwa, zama za kuficha mambo zimemalizika na filihali, utambulisho wa kweli wa Saudi Arabia umefahamika wazi  na bayana mbele ya fikra za waliowengi katika Mashariki ya Kati na ulimwengu kwa ujumla.

Mfalme Salman bin Abdul-Aziz wa Saudi Arabia

Abdel Bari Atwan, mwandishi mashuhuri na mhariri mkuu wa gazeti la Rai al-Youmwa anasema akitoa tathmini yake kuhusiana na suala hili kwamba:

..."Israel inafuatilia kuipeleka Saudi Arabia na kuitumbukiza katika vita mtawalia ambayo vitaipeleka Riyadh na eneo la Mashariki ya Kati upande wa uharibifu. Mbali na kuharibiwa vyanzo vya utajiri, vita hivyo vitasababisha kutokea ukosefu wa amani na uthabiti na kubwa zaidi ni kuleta migawanyiko ndani ya nchi hizo.

Hatua ya Saudi Arabia ya kuunga mkono magaidi, kuanzisha vita dhidi ya Yemen na kuzua migogoro katika Mashariki ya Kati imeifanya nchi hiyo kuhudumia malengo ya Marekani na utawala haramu wa Israel. Utendaji huo wa Saudi Arabia umekuwa chimbuko la kuongezeka na kushadidi migogoro katika Mashariki ya Kati.

Nchi yenye faili jeusi kama hii, katu haiwezi kujinasua kutoka katika kinamasi ilichokwama na kufikia malengo yake katika eneo la Mashariki ya Kati kupitia uenezaji uongo unaofanywa na viongozi wake dhidi ya mataifa mengine.

Maoni