• Msimamo wa Theresa May wa kuitetea Israel, harakati ya kufuata nyayo za Trump

Serikali ya Kihafidhina (Conservative) ya Uingereza inahesabiwa kuwa miongoni mwa watetezi na waungaji mkono wakubwa wa utawala wa Kizayuni wa Israel na licha ya jinai na uhalifu mkubwa unaofanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Palestina, lakini hakushuhudiwi mabadiliko ya aina yoyote katika mienendo ya London katika uwanja huu.

Uingereza pia haijachukua msimamo wa maana kuhusu mauaji yanayofanywa na Israel dhidi ya raia wa Palestina hususan katika eneo la Ukanda wa Gaza katika maandamano yanayofanyika kila siku ya Ijumaa. Vilevile inaendelea kuuuzia utawala huo katili silaha zinazotumika kuua raia wasio na hatia yoyote. 

Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May pia ameamua kuchukua msimamo tofauti na ule wa Umoja wa Ulaya ambao umelaani vikali hatua ya Israel ya kuafukuza Wapalestina katika kijiji chao cha Khan al Ahmar huko katika Ukingo wa Magharibi. Theresa May ameungana na Rais wa Marekani, Donald Trump aliyetangaza uungaji mkono kamili kwa Israel katika jinai hiyo iliyolaaniwa na jamii nzima ya kimataifa. 

Jioni ya Jumatatu iliyopita May alihutubia kikao cha muungano unaoitwa "Mayahudi wa Israel" na kusisitiza kwamba ataendelea kupambana na kile alichokiita chuki dhidi ya Mayahudi na kuiunga mkono Israel. Theresa May ameongeza kuwa, katika kipindi chote cha uongozi wake kama waziri mkuu wa Uingereza nchi hiyo daima imekuwa mshirika wa kuaminika wa utawala huo na itaendelea kuwa hivyo. 

Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu na mwenzake wa Uingereza, Theresa May.

Waziri Mkuu wa Uingereza pia ameshiria uhusiano mkubwa na wa kina wa London na Tel Aviv na kutilia mkazo kauli hiyo kwa kuashiria masuala kadhaa kama sherehe za kutumia miaka 100 tangu baada ya Azimio la Balfour lililopelekea kuasisiwa dola haramu la Israel katika ardhi ya Palestina na safari iliyofanywa hivi karibuni na mwanamfalme William, mjukuu wa Malikia Elizabeth wa Uingereza huko Israel.  

Waziri Mkuu wa Uingereza ambaye ameamua kuonesha waziwazi jinsi anavyofuata kibubusa sera za Donald Trump na utawala wa katili wa Tel Aviv, ametilia mkazo kile alichodai ni haki ya Israel ya kujilinda! Hata hivyo May hakuashiria hata kidogo mashambulizi ya kinyama na mauaji yanayofanywa kila siku ya askari wa Israel huko Palestina ambayo yanaendelea kulaaniwa na walimwengu. Vilevile amesahau au kujisahaulisha upinzani mkubwa wa Waingereza wanaolalamikia ushawishi mkubwa wa Wazayuni wa Israel katika siasa za nchi yao.

Itakumbukwa kuwa hivi karibuni zaidi ya Waingereza elfu kumi walisaini hati wakiitaka serikali ya Theresa May ishughulikie suala la ushawishi wa utawala wa Kizayuni wa Israel katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.

Baadhi ya Waingereza wakipinga safari ya Netanyahu..

Uingereza imezidisha uuzaji wa silaha kwa Israel licha ya kuongezeka mauaji na ukandamizaji wa utawala huo dhidi ya raia wasio na hatia wa Palestina. Mwaka uliopita wa 2017 London iliidhinisha mauzo ya siha zenye thamani ya pauni milioni 221 kwa utawala katili wa Israel unaotambuliwa kuwa soko kubwa la 8 la makampuni ya silaha ya Uingereza. Uingereza, Marekani na Ujerumani ni miongoni mwa wauaji wakuu wa silaha kwa Israel. Kwa kutilia maanani ukweli huo, hivi karibuni kiongozi wa chama cha Leba, Jeremy Corbyn aliitaka serikali ya London kutazama upya suala la kuuuzia silaha utawala haramu wa Israel ambazo zinatumika kukiuka sheria za kimataifa.

Andrew Smith ambaye ni mjumbe katika kampeni ya kupinga biashara ya silaha anasema: "Silaha zinazotengenezwa nchini Uingereza zinatumiwa dhidi ya raia wa Palestina kwa ruhusa ya serikali ya London." 

Wapalestina wanaendelea kuuliwa kwa silaha za Uingereza na Marekani.

Itakumbukwa pia kwamba, Uingereza iliunga mkono na kukingia kifua mashambulizi ya utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza mwaka 2008, 2012 na 2014.

Hii ni pamoja na kwamba, mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu yanaitambua Israel kuwa ni mkukaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu duniani na inaendelea kuua raia wa Palestina hususan katika eneo la Ukanda wa Gaza.

Tags

Sep 19, 2018 06:36 UTC
Maoni