• ICC yaanza kuchunguza jinai za Myanmar dhidi ya Waislamu Warohingya

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imeanza kuchunguza jinai dhidi ya binaadamu zinazofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya.

Taarifa iliyotolewa na Fatou Bensouda, Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC imesema korti hiyo yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi imeanzisha uchunguzi wa awali wa kubaini iwapo kuna ushahidi wenye mashiko ambao utatoa waranti wa kuanzisha uchunguzi kamili kuhusu jinai za jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya, yakiwemo mauaji, ubakaji na kufukuzwa makwao watu wa jamii hiyo ya wachache katika nchi hiyo ya kusini mashariki mwa bara Asia.

Tangazo hilo la ICC limetolewa katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa hapo jana Jumanne pia ulisisitizia haja ya kufunguliwa mashitaka makamanda waandamizi wa jeshi la Mynamar kutokana na mauaji ya kizazi dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya. 

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limekuwa likisisitiza kuwa, jeshi la Myanmar linawaua kiholela na kuwanajisi Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa nchi hiyo.

Sehemu ndogo ya jinai za Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka jana hadi sasa. 

Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar yamepelekea zaidi ya nusu milioni kati yao kukimbilia hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Tags

Sep 19, 2018 06:43 UTC
Maoni