Sep 24, 2018 14:02 UTC
  • Amnesty: China imetenganisha malaki ya familia za Waislamu

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International sambamba na kulaani ukandamizaji unaofanywa na vyombo vya usalama dhidi ya Waislamu nchini China, limesema kuwa mamia ya maelfu ya familia za Waislamu nchini humo zimelazimika kutengana na jamaa zao kutokana na dhulma hizo za serikali.

Nicholas Bequelin, Mkurugenzi wa Amnesty katika eneo la Asia Mashariki amesema leo Jumatatu kuwa, "Familia hizo za Waislamu zimegubikwa na wahaka mkubwa zikitaka kujua waliko wapendwa wao. Wakati umefika vyombo vya dola viwape maelezo na kuwafafanunulia watu hao kuhusu jamaa zao."

Katika ripoti yake mpya, Amnesty International imesema ina ushahidi kutoka kwa baadhi ya Waislamu waliozuiliwa katika vituo vya serikali na pia kutoka mashirika ya kutetea haki za binadamu, unaoonesha kuwa, hatua za kiusalama zimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni nchini China haswa ndani ya mkoa wa Xinjiang, maghairibi mwa nchi.

Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa ukieleza wasiwasi wake juu ya siasa za ukandamizaji zinazotekelezwa na serikali ya Beijing katika kuamiliana na jamii ya Waislamu wa nchi hiyo.

Polisi wakikata vazi refu la mwanamke Muislamu China

Inafaa kuashiria kuwa, serikali ya Beijing na kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, imeanzisha vituo kadhaa katika mkoa wa Xinjiang ambavyo vimekuwa vikitumika kuwazuilia Waislamu.

Hii ni katika hali ambayo serikali ya China imetoa ripoti kadhaa ikipinga ripoti ya timu ya Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu, iliyothibitisha kwamba karibu Waislamu milioni moja wanazuiliwa na maafisa usalama wa nchi hiyo.

Tags

Maoni