Sep 25, 2018 06:17 UTC
  • Malalamiko makali ya Jeremy Corbyn kwa kitendo cha UK cha kuipa silaha Saudia

Nchi ya Saudi Arabia inayotawaliwa na ukoo mmoja, mwezi Machi 2015 ilianzisha vita vya pande zote dhidi ya nchi maskini ya Yemen kwa kushirikiana na waitifaki wake hasa Umoja wa Falme za Kiarabu.

Uingereza pamoja na Marekani zina nafasi kubwa sana katika vita hivyo kutokana na kutoa misaada ya kilojistiki kama kuyapa silaha madola hayo vamizi, msaada wa taarifa za kijasusi na misaada mingine ya kijeshi. Katika miaka ya hivi karibuni, Uingereza imeelekeza nguvu zake katika kutia saini mikataba mingi zaidi ya kijeshi na ukoo wa Aal Saud kiasi kwamba hivi sasa utawala wa Saudia ndiye mnunuzi mkubwa zaidi wa silaha za Uingereza. Hata hivyo, siasa hizo za chama cha Kihafidhina cha Uingereza zimekumbwa na malalamiko makubwa ya mashirika na taasisi za haki za binadamu ndani na nje ya nchi hiyo. 

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May katika uhusiano wa karibu na wavamizi wa Yemen

 

Jeremy Corbyn, mkuu wa chama cha Leba cha nchi hiyo amelalamikia vikali nafasi ya London katika kuushehenesha silaha utawala wa Aal Saud unaotenda jinai nchini Yemen na kusema kuwa, serikali ya Britania ina wajibu wa kuacha kuipa silaha Saudi Arabia ili kwa njia hiyo iulazimishe ukoo wa Aal Saud uache jinai zake nchini Yemen.

Corbyn amesema hayo mbele ya jamii ya Wayemen waishio mjini Liverpool, Uingereza na kuongeza kuwa, kama chama cha Leba kitafanikiwa kuunda serikali, basi kesho yake tu kitapeleka muswada kwa Umoja wa Mataifa wa kutaka kukomeshwa vita nchini Yemen.

Kwa upande wake, gazeti la Independent la nchini Uingereza limeripoti kuwa, idadi ya mabomu na makombora yaliyotengenezwa Uingereza na ambayo yanatumiwa na Saudi Arabia katika vita huko Yemen, imeongezeka kwa asilimia 500 tangu kuanza vita hivyo vya kivamizi. Katika kipindi cha miaka miwili ya kuanza vita vya Yemen, London iliiuzia Saudia silaha zenye thamani ya zaidi ya Pound bilioni nne na milioni 600, na licha ya kuweko ushahidi mwingi wa kuthibtisha kuwa Saudia inatumia silaha hizo kufanya jinai za kivita, lakini serikali ya Britania imezidi kutoa idhini ya kuuziwa silaha Riyadh.

Wahanga wakubwa wa jinai zinazofanywa na Saudia kwa silaha inazopewa na nchi za Magharibi hasa Marekani na Uingereza, ni watoto wadogo wa Yemen

Licha ya kutolewa ripoti nyingi kuhusu kuuliwa idadi kubwa ya raia huko Yemen katika mashambulizi ya anga yanayofanywa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia, lakini serikali ya kihafidhina huko London inaendelea kukaidi mwito wa ndani na nje ya Uingereza wa kuitaka iache kuuzia silaha ukoo wa Aal Saud. Sergey Syberibov, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Russia amesema, Marekani na Uingereza zinapata fedha nyingi kutokana na vita vya Yemen.

Ukweli wa mambo ni kuwa nchi za Magharibi zinafanya kila njia kuhakikisha kuwa tawala za kiimla zinazokubali kuburuzwa na Magharibi zinaendelea kubakia madarakani kwa thamani yoyote ile. Hivi sasa Uingereza ina nafasi kubwa katika kutoa mafunzo ya kijeshi kwa wanajeshi wa Saudi Arabia bali hata katika kuziandaa na kuziweka tayari ndege za kivita za Tornado kabla ya Saudia kwenda kufanya mauaji nchini  Yemen.

Jeremy Corbyn, mkuu wa chama cha Leba cha nchini Uingereza

 

Serikali ya kihafidhina ya Britania si tu kwamba inafumbia macho uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na Saudia, lakini hata inashiriki katika jinai hizo. Ripoti ya taasisi ya kuwahami watoto wadogo vitani ya nchini Uingereza imeyatuhumu mashirika ya kutengeneza silaha ya Britania kwa kukomba utajiri mkubwa kutokana na mauaji wanayofanyiwa watoto wadogo wasio na hatia huko Yemen.

Alaakullihaal, kadiri vita vya Yemen vinavyoendelea ndivyo unafiki na undumilakuwili wa Uingereza unavyozidi kufichuka. Kwa upande mmoja, London inaiuzia silaha Saudia na kuwapa mafunzo wanajeshi wake lakini kwa upande wa pili, London hiyo hiyo inadai kuwa eti inaunga mkono utatuzi wa kisiasa wa mgogoro wa Yemen.

Maoni