Sep 25, 2018 08:11 UTC
  • Marekani kuiuzia Taiwan silaha za kijeshi za dola milioni 330

Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imesema serikali ya Washington imeidhinisha mauzo ya silaha za kijeshi kwa Taiwan yenye thamani ya dola milioni 330.

Idara ya Ushirikiano wa Usalama na Ulinzi ya Pentagon imebainisha kuwa, katika kuimarisha uhusiano wa kijeshi kati ya Marekani na Taiwan, Washington imekubali kuliuzia eneo hilo ambalo China inadai ni milki yake vipuri vya ndege za kijeshi aina ya F-16, C-130, F-5 miongoni mwa zana zingine za kijeshi.

Wataalamu wa masuala ya kijeshi wanasema hatua hiyo ya Washington kuendelea kurundika silaha Taiwan itashadidisha uhasama kati ya Marekani na China, ambazo wakati huu zipo katika vita vikubwa vya kibiashara.

Inafaa kuashiria kuwa, katika miaka ya hivi karibuni na katika kutekeleza mpango wa kuongeza uwezo wake wa kijeshi, serikali ya Taiwan imefunga mikataba kadhaa ya ununuzi wa silaha kutoka Marekani, kitendo ambacho pia kimekuwa kikilalamikiwa na Beijing.

Kuvurugika uhusiano kati ya China na US

Mapema mwaka huu, China iliionya Washington kwamba, kitendo chake cha kuvuka mipaka ya China na kufanya mawasiliano na viongozi wa eneo la Taiwan, hakitakuwa na faida yoyote ghairi ya kuharibu mahusiano kati ya Marekani na China.

China inaitambua Taiwan ambayo mwaka 1949 ilijitenga na nchi hiyo baada ya vita vya ndani, kuwa ni sehemu ya ardhi yake. 

Tags

Maoni