Oct 10, 2018 07:59 UTC
  • Takwa la Ujerumani la kuasisiwa Baraza la Usalama la Umoja wa Ulaya

Kuibuka hitilafu na mizozo mikubwa baina ya Marekani na Umoja wa Ulaya baada ya kuingia madarakani Rais Donald Trump hususan katika masuala ya kiulinzi, nafasi na umuhimu wa Shirika la Kijeshi la NATO sambamba na kujitoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya (Brics) ni mambo ambayo yamezifanya nchi wanachama wa EU zichukue hatua za kuimarisha mipango na mikakati ya kujitegemea katika uga wa ulinzi na usalama.

Katika uwanja huo, kumefanyika juhudi kubwa kwa ajili ya kuanzisha kikosi huru na kinachojitegemea cha ulinzi cha Ulaya, kuandaliwa mkakati wa kimataifa wa Umoja wa Ulaya na kadhalika kuanzishwa taasisi za kijeshi na kiulinzi za Ulaya. Ujerumani na Ufaransa zikiwa nchi mbili muhimu wanachama wa Umoja wa Ulaya zimekuwa mstari wa mbele katika mchakato huo.

Madola hayo mawili ya Ulaya yanataka Umoja wa Ulaya uwe na uwezo wake usio tegemezi wa kiulinzi haraka iwezekanavyo sambamba na kuimarisha na kuweko  mwelekeo wa pamoja wa kiulinzi barani Ulaya. 

Heiko Maas, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani

Juni 18 mwaka huu, Ufaransa na Ujerumani zilitoa pendekezo la kuasisiwa asasi mpya kwa ajili ya kufuatilia masuala ya pamoja ya kiusalama na ya nje ya bara hilo. Nchi 9 za Ulaya, ziliunga mkono mpango huo wenye lengo la kuanzisha kikosi cha radiamali ya haraka. Kwa mujibu wa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ambaye anataka kuhitimishwa utegemezi wa Ulaya kwa uungaji mkono wa kijeshi wa Marekani ni kuwa, Umoja wa Ulaya unapaswa kuwa na 'mkakati huru na usio tegemezi' katika uga wa ulinzi.

Katikka upande mwingine, Heiko Maas Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ujerumani alisisitiza mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu juu ya kuimarishwa ushirikiano wa kijeshi na ''kuunda nguvu na kambi" kwa ajili ya kukabiliana na Marekani, hata hivyo hilo sio pendekezo la mwisho la Ujerumani. Aidha katika matamshi yake ya hivi karibuni aliyoyatoa Oktoba nane mwezi huu, Heiko Maas anataka kuanzishwa taasisi mpya ya Ulaya yaani Baraza la Usalama la Umoja wa Ulaya.

Kwa mujibu wa waziri huyo wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani ni kuwa, kuasisiwa Baraza la Usalama la Umoja wa Ulaya kunaweza kuwa jibu bora na la mahala pake kwa migogoro ya  kimataifa. Katika fremu hiyo, kundi dogo la wanachama kwa uwakilishi wa Umoja wa Ulaya linaweza kutoa jibu la haraka na athirifu kwa migogoro ya sasa.

Jean-Claude Juncker, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya

Serikali ya Ujerumani inaamini kwamba, wanachama wa Umoja wa Ulaya wanapaswa kuwa na utendaji mpya kwa ajili ya kuchukua maamuzi katika masuala ya sera za kigeni. 

Jean-Claude Juncker, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya naye ametaka kurahisishwa mchakato wa uchukuaji maamuzi katika sera za usalama na ulinzi za umoja huo. Kwa kuzingatia mizozo na hitilafu zilizoibuka na zinazoongeza kila leo baina ya Umoja wa Ulaya na Marekani, hivi sasa uga wa ulinzi na sera za kigeni kwa Umoja wa Ulaya na kuwa na uhuru na mamlaka kamili ni jambo lenye umuhimu mkubwa. Kuwa na uhuru kamili katika suala la ulinzi maana yake ni kupunguza utegemezi kwa Marekani katika kuilinda Ulaya. 

Katika uwanja huo, Disemba mwaka jana nchi 25 za Umoja wa Ulaya zilipasisha suala la 'muundo wa kudumu wa ushirikiano katika usalama na ulinzi wa Umoja wa Ulaya (PESCO), hatua ambayo inafungua ukurasa zaidi wa ushirikiano wa nchi wanachama katika nyuga za ulinzi na usalama.

Misimamo hasi ya Rais Donald Trump wa Marekani ambaye nchi yake ni mwanachama muhimu wa Shirika la Kijeshi la NATO dhidi ya taasisi hiyo ya kijeshi, imezifanya nchi za Ulaya kuutazama kwa jicho la shaka mustakbali wa NATO. Umoja wa Ulaya ulitangaza Mei mwaka huu kwamba, kuanzia mwaka 2021 hadi 2027 itatenga kiasi cha Euro bilioni 20 kwa ajili ya masuala ya ulinzi na kwamba, bajeti hiyo ya fedha itatumika kupanua teknolojia mpya kijeshi.

Rais Donald Trump wa Marekani

Kwa hakika madola ya Ulaya yamefikia natija hii kwamba, filihali yanapaswa kujitegemea na kwamba, kipindi cha nchi hizo kuwa tegemezi kwa Marekani kwa ajili ya kulinda usalama wa Ulaya kimepita na kumalizika.  Rais Trump ametangaza na kusisitiza kinagaubaga kwamba, Marekani haiko tayari tena kuwapatia lifti washirika wake. Marekani si tu kwamba, inataka washirika wake wa Ulaya wabebe mzigo wa gharama za ulinzi, bali inataka pia ifaidike na kunufaika na uhusiano wake na madola hayo. 

Harakati na hatua za Ulaya za kutaka kujitegemea kiulinzi na kijeshi ambapo moja ya malengo yake ni kuupa nguvu Umoja wa Ulaya ya kukabiliana na migogoro ya kiusalama ndani ya bara hilo, zimezidi kuikasirisha Marekani, kwani kufanikiwa hilo maana yake ni kupungua uwezo na nguvu ya Washington ya kuingilia na kuwa na nafasi muhimu katika migogoro ya kiusalama ya Ulaya.

Tags

Maoni