Oct 16, 2018 08:10 UTC
  • CNN na NBC: Saudia itakiri kumuua Khashoggi, itamsafisha Bin Salman

Vyombo vya habari vya Marekani vimetangaza kuwa, serikali ya Saudi Arabia inajitayarisha kukiri kwamba imemuua mwandishi na mkosoaji wa utawala wa nchi hiyo, Jamal Khashoggi katika ubalozi wake mjini Istanbul kwa njia ambayo itamsafisha na kumuondoa hatiani mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo Muhammad bin Salman.

Televisheni ya CNN ya Marekani imewanukuu maafisa wa nchi hiyo wakisema Saudi Arabia inatayarisha ripoti itakayokiri kuuawa Khashoggi kimakosa wakati wa kusailiwa ndani ya ubalozi wa nchi hiyo mjini Istanbul katika operesheni ya kujaribu kumteka nyara.

Vyombo vya habari vya Marekani vimesema ripoti hiyo ya Saudia itasisitiza kuwa operesheni hiyo imefanyika bila ya idhini ya serikali ya Saudia na kwamba waliohusika watachukuliwa hatua. Chombo kilichovujisha habari hiyo kimesema kuwa, ripoti hiyo bado inaandaliwa na kwamba yumkini kukafanyika mabadiliko katika utayarishaji wake.

Televisheni ya NBC pia imefichua kwamba, Saudia inatayarisha ripoti itakayokiri kuuawa Khashoggi ndani ya ubalozi wa nchi hiyo huko Uturuki lakini itamsafisha Muhammad bin Salman na mauaji hayo ikisisitiza kuwa, hakutoa amri ya kuuawa Jamal Khashoggi wala hakuwa na habari kuhusu mauaji yake.

Muhammad bin Salman

Mwandishi na mkosoaji wa serikali ya kifalme ya Saudi Arabia Jamal Khashoggi alitoweka tarehe Pili mwezi huu baada ya kuingia ndani ya ubalozi wa nchi hiyo mjini Istanbul, Uturuki. Baadaye vyombo vya habari viliwanukuu baadhi ya maafsia wa serikali ya Uturuki wakisisitiza kuwa mwandishi huyo aliuawa ndani ya ubalozi huo na mwili wake ukakatwa vipande vipande.

Maoni