Oct 23, 2018 03:00 UTC
  • Russia yakanusha madai ya Marekani kuhusu mkataba wa makombora ya nyuklia

Msemaji wa Rais wa Russia amesema kuwa madai yanayotolewa na Marekani dhidi ya Russia kwamba imekiuka mkataba wa silaha za nyuklia za masafa ya kati ni urongo na hayana msingi wowote.

Dmitry Peskov amesema Russia imeheshimu vipengee vya mkataba huo na kuongeza kuwa, uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu suala la kujiondoa serikali ya Washington katika mkataba huo unatia wasiwasi na maamuzi kama hayo yanahatarisha usalama na amani ya dunia. 

Hata hivyo Peskov amesema, hadi sasa Marekani haijachukua hatua yoyote ya kujiondoa kwenye mkataba huo na kwamba kuna taratibu kadhaa zinazopaswa kufuatwa kabla ya kujiondoa kwenye makubaliano huo. 

Msemaji wa Rais wa Russia ameongeza kuwa, uamuzi wa Marekani wa kujiondoa katika mkataba wa silaha za nyuklia za masafa ya kati utajadiliwa katika mazungumzo ya maafisa wa serikali ya Moscow na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani John Bolton mjini Moscow. 

Jumamosi iliyopita Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa, Washington inajitayarisha kujiondoa katika mkataba wa silaha za nyuklia za masafa ya kati INF kwa kifupi, wiki ijayo. 

Trump: Marekani itajiondoa katika mkataba wa nyuklia wa INF.

Mkataba INF ulitiwa saini mwaka 1987 mjini Washington na kuanza kutekelezwa mwaka 1988. Mkataba huo wa silaha za nyuklia za masafa ya kati unazizuia nchi hizo mbili kuweka makombora ya balestiki na ya Cruise barani Ulaya. Mkataba huo pia unasisitiza ulazima wa kuharibiwa makombora ya nyuklia ya masafa ya kati ya kilomita 1000 mpaka 5500 na yale ya masafa mafupi ya kilomita 500 hadi 1000. 

Tags

Maoni