Oct 23, 2018 03:03 UTC
  • Kushadidi radiamali za Ulaya dhidi ya jinai za Saudi Arabia

Utawala wa Saudi Arabia ambao daima umekuwa ukijifakharisha kuwa na uhusiano mzuri na madola ya Magharibi, filihali unakabiliwa na changamoto ambayo haijawahi kushuhudiwa katika uga wa kimataifa.

Changamoto hiyo inatokana na mauaji ya Jamal Khashoggi mwandishi wa habari na mkosoaji maarufu wa utawala wa Aal Saud ambaye aliuawa katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul Uturuki. Fikra za waliowengi ulimwenguni na mataifa mbalimbali ya dunia yanataka kuwekwa wazi na kueleweka bayana kadhia ya Khashoggi. Wakati huo huo, hivi sasa kunashuhudiwa kuongezeka radiamali mbalimbali katika uga wa kimataifa dhidi ya jinai za Aal Saud. Katika fremu hiyo, waitifaki wa  Ulaya wa Saudi Arabia wamechukua msimamo mpya katika uwanja huo huku baadhi yao wakichukua hatua za kushadidisha mashinikizo dhidi ya Riyadh.

Jumamosi iliyopita na baada ya kupita wiki mbili za mashinikizo mazito ya vyombo vya habari, hatimaye Saudi Arabia ilikiri wazi kwamba, Jamal Khashoggi aliuawa katika ubalozi wa nchi hiyo huko Istanbul Uturuki. Hata hivyo, Saudia ilidai kuwa, Khashoggi aliuawa baada ya kuibuka mapigano baina yake na maafisa wa ubalozi ndani ya ubalozi huo na kwamba, Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha Saudi Arabia hakuhusika kwa namna yote na kifo cha mwendazake Jamal Khashoggi.

Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoaji mkubwa wa Saudi Arabia aliuawa katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul

Katika uwanja huo, nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani siku ya Jumapili zilitoa taarifa rasmi zikilaani mauaji ya mwanahabari huyo na kusisitiza kwamba, hakuna kisingizio chochote kinachoweza kuhalalisha mauaji ya Khashoggi. Sehemu moja ya taarifa ya nchi hizo tatu za Ulaya ambayo imewekwa katika kurasa za mitandao za wizara hizo imeeleza kuwa, licha ya kuwa kwa siku kadhaa kulikuwa na hofu ya kuuawa kinyama Jamal Khashoggi ndani ya ubalozi mdogo wa Saudi Arabia huko Istanbul, lakini kuthibitishwa mauaji hayo nako kumeshtusha sana.

Nchi hizo zimeitaka Saudi Arabia ifanye uchunguzi na kuwashughulikia kisheria wale wote waliohusika na jinai hiyo. Aidha nchi hizo za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimesisitiza kwamba, namna na umuhimu wa uhusiano wetu na Mfalme wa Saudia umejengeka juu ya msingi wa heshima na sisi sote na viongozi wa Riyadh tunaheshimu thamani chini ya sheria za kimataifa.

Kwa hakika madola ya Ulaya yameionya Saudi Arabia kwamba, kuendelea mwenendo wa sasa yaani wa Riyadh kufanya juhudi za kuficha ukweli na kuhalalisha mauaji ya Khashoggi, ni jambo ambalo linaweza kuwa na taathira hasi katika uhusiano wa Ulaya na nchi hiyo ya Kiarabu.

Muhammad bin Salman mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia ambaye inasemekana alitoa amri ya kuuawa Jamal Khashoggi

Tab'an, sababu ya msimamo huo iko wazi nayo ni kwamba, madola ya Ulaya yana habari kamili kuhusiana na utendaji wa Saudi Arabia katika suala zima la haki za binadamu. Kama ambavyo madola hayo, mara kadhaa yameshuhudia taarifa na malalamiko ya jumuiya na asasi za kimataifa za haki za binadamu kuhusiana na jinai za kutisha za Saudia katika vita dhidi ya wananchi madhulumu wa Yemen.

Kwa muktadha huo, tunaweza kutathmini msimamo huo wa Ulaya kwamba, zaidi unatokana na mashinikizo ya fikra za waliowengi barani Ulaya na katika ulimwengu wa Magharibi dhidi ya tawala hizo ambazo zimekuwa zikiuuzia silaha za kila aina utawala wa Aal Saud. Hapana shaka kuwa, kama nchi hizo hazitaonyesha radiamali dhidi ya jinai za Saudi Arabia, hatua hiyo itakuwa na matokeo mabaya kwa tawala za nchi hizo hasa serikali ya muuungano ya Ujerumani na ile ya wahafidhina ya nchini Uingereza.

Yumkini ni kwa sababu hiyo ndio maana Jumapili iliyopita, Kansela wa Ujerumani Bi Angela Merkel sambamba na kulaani kuuawa Jamal Khashoggi akatangaza kuwa, Berlin imesimamisha kuiuzia silaha Riyadh mpaka pale faili la mauaji ya Khashoggi na utata uliopo kuhusiana na tukio hilo utakapobainika na kufahamika kinagaubaga.

Bi Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani

Hivi sasa Saudi Arabia iko njia panda ambapo mbele yake kuna njia mbili. Njia ya kwanza ni iendelee kukana kuhusika kwake katika mauaji hayo. Na inavyoonekana itachagua njia ya pili nayyo ni ya kukiri kuhusika kikamilifu na mauaji ya mwandishi huyo hasa kwa kutilia maanani mashinikizo ya kimataifa yanayoongezeka kila leo dhidi ya nchi hiyo.

Hivi sasa tunasubiri kuona haya madola yya Magharibi yanayodai kutetea haki za binadamu yatauchukulia hatua gani utawala wa Aal Saud. Tajiriba ya huko nyuma inaonyesha kuwa, siku zote madola hayo yamekuwa yakifumbia macho ukiukaji wa haki za biandamu unaofanywa na Saudi Arabia na kuamua kutanguliza mbele suala la kupanua ushirikiano wao na Riyadh hasa katika uga wa kijeshji na silaha.

Tags

Maoni