Oct 23, 2018 13:33 UTC
  • UN yakosoa hatua ya Ufaransa ya kupiga marufuku burqa

Kamati ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeijia juu serikali ya Ufaransa kwa kupiga marufuku vazi la stara la burqa linalovaliwa na baadhi ya wanawake Waislamu nchini humo.

Imesema marufuku hiyo inakiuka moja kwa moja haki za wanawake Waislamu nchini humo, na kwamba wale waliopigwa faini kwa kuvaa vazi hilo wanapaswa kurejeshewa fedha zao.

Kamati hiyo imesema haijaridhishwa na hoja ya serikali ya Ufaransa, kwamba imepiga marufuku vazi hilo la staha katika maeneo ya umma kwa misingi ya kiusalama na kijamii.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Yuval Shany amesema hatua hiyo ya Ufaransa ya kupiga marufuku vazi la niqabu haijazingatia mlingano baina ya maslahi ya umma na haki za mtu binafsi. 

Nchi nyingi za EU zimepiga marufuku vazi la burqa

Kwa mujibu wa sheria hiyo, yeyote atakayevaa vazi hilo la stara katika maeneo ya umma atatozwa faini ya Euro 150 sawa na dola 170 za Marekani.

Ufaransa ilijiunga na baadhi ya nchi za Magharibi zilizopiga marufuku vazi la burqa kama vile Canada, Ubelgiji, Uholanzi na Bulgeria, baada ya bunge la nchi hiyo kupasisha sheria inayopiga marufuku vazi hilo linalovaliwa na baadhi ya wanawake Waislamu nchini humo.

Tags

Maoni