Nov 13, 2018 14:43 UTC
  • Korea Kusini yakadhibisha ripoti ya taasisi ya kifikra ya Marekani kuhusu Korea Kaskazini

Ofisi ya Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini imekadhibisha ripoti ya taasisi ya kifikra ya Marekani ya 'Kituo cha Utafiti wa Kimataifa na Kistratijia' juu ya kuendelea shughuli za makombora ya siri ya Korea Kaskazini.

Taarifa hiyo ya ofisi ya rais wa Korea Kusini imetolewa ikiwa imepita siku moja baada ya kutolewa ripoti ya taasisi hiyo ya kifikra ya Marekani juu ya kuendelea shughuli za makombora ya balestiki nchini Korea Kaskazini katika maeneo 16 ya siri ya nchi hiyo. Katika taarifa hiyo, ofisi ya Rais Moon Jae-in imesema kuwa, taarifa ya 'Kituo cha Utafiti wa Kimataifa na Kistratijia' ni ya kupindukia na iliyozidisha mambo. Awali ripoti ya kituo hicho ilidai kwamba, nyaraka za kuthibitisha jambo hilo zilitokana na picha za satalaiti na mazungumzo yaliyofanywa kwa kuwahoji wakimbizi wa Korea Kaskazini, maafisa usalama na wa ulinzi wa nchi hiyo.

Ofisi ya Rais  Moon Jae-in wa Korea Kusini iliyopinga taarifa hiyo

Wakati huo huo Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini imesisitiza kuendeleza maneva ya kijeshi ya baharini kati yake na Marekani licha ya upinzani mkubwa wa serikali ya Pyongyang. Taarifa iliyotolewa na wizara hiyo imesema kuwa, serikali ya Korea Kusini haiwezi kusitisha maneva yake hayo ya kijeshi kutokana na ukosoaji wa Korea kaskazini. Imeongeza kwamba maneva hayo yaliyoanza wiki iliyopita na ambayo yanatazamiwa kuendelea kwa wiki nyingine ijayo, ni ya kiulinzi tu. Maneva hayo kati ya Marekani na Korea Kusini yamekuwa yakifanyika tangu miaka ya huko nyuma, hata hivyo yalisimamishwa kwa muda kutokana na serikali za Korea mbili kutiliana saini makubaliano ya pande mbili yenye lengo la kupunguza mzozo baina yao na baada ya kukutana viongozi wa juu wa Korea Kaskazini na Marekani.

Tags

Maoni