Nov 18, 2018 02:47 UTC
  • Kura ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya Syria ya kumiliki eneo la Golan licha ya upinzani wa Marekani

Rasimu ya "Azimio la Golan" iliyopasishwa siku ya Ijumaa kwa kura nyingi katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika mjini New York imethibitisha tena kwamba eneo la Golani ni milki ya Syria.

Nchi 151 zililipigia kura za ndio azimio hilo hilo. Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel pekee zilipiga kura ya kupinga rasimu hiyo ya "Azimio la Golan". Azimio hilo linathibitisha kuwa  eneo la Golan linalokaliwa kwa mabavu na Israel ni milki ya Syria na imezitaja hatua zote za utawala wa Kizayuni katika eneo hilo kuwa ni batili na kinyume cha sheria. Utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 1967 ulivamia na kulikaribia kwa mabavu eneo la ardhi ya Syria la karibu kilomita mraba 1200 pamoja na miinuko ya Golan na baada ya kupita muda utawala huo ukaliunganisha eneo hilo na ardhi inazozikalia kwa mabavu.  Jamii ya kimataifa kamwe haitambui rasmi hatua hiyo ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Miinuko ya Golan ipo kusini magharibi mwa Syria katika mkoa wa Qunaitra na tangu mwanzoni mwa kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina eneo hilo lilitiliwa maanani na utawala wa Kizayuni kwa kuzingatia umuhimu wake wa kijiografia, kisiasa na kistratejia. Miinuko ya Golan ipo katika eneo linalopakana na nchi za Lebanon, Jordan, na Palestina na mazingira yake yanayolifanya eneo hilo kuwa juu ya miji ya Damascus, Beirut, Tel Aviv na Amman ni miongoni mwa sababu zinazoifanya Israel ing'ang'anie  eneo hilo. Katika fremu hiyo utawala wa Kizayuni  unatumia hila na mbinu mbalimbali ili kufanikisha siasa zake za kuendelea kuwepo katika maeneo iliyoyavamia na kuyakalia kwa mabavu likiwemo eneo la Golan huko Syria ikiwa ni pamoja na kutumia njia ya kubadili muundo wa kijamii na utambulisho wa mipaka ya miinuko ya eneo hilo.

Kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ni utawala ghasibu na vamizi umezuiwa kuchukua hatua yoyote yenye lengo la kubadili muundo wa kijamii na ule wa kijografia wa maeneo unayoyakalia kwa mabavu. Hatua hizo za kupenda kujitanua za Israel huko Syria na matamshi ya viongozi wa utawala huo ya kuendelea kulikalia kwa mabavu eneo la Golan yanatolewa katika hali ambayo ni kwa miaka kadhaa sasa ambapo Syria imetumbukia katika mgogoro mkubwa wa ndani kutokana na njama za Wamagharibi, Uzayuni wa kimataifa na vibaraka wao katika eneo la Mashariki ya Kati. Fitna na njama hizo dhidi ya Syria zinatekelezwa kwa lengo la kuidhoofisha nchi hiyo ili isalimu amri mbele ya siasa za kujitanua za utawala wa Kizayuni na za nchi za Magharibi katika Mashariki ya Kati. 

Eneo la miinuko ya Golan nchini Syria 

Baada ya kunza machafuko ya Syria mwezi Machi mwaka 2011 utawala wa Kizayuni wa Israel, tawala za Magharibi zinazouunga mkono utawala huo ghasibu na baadhi ya tawala za Kiarabu zilizusha mapigano ya ndani nchini Syria kwa kupanda mawimbi ya malalamiko ya baadhi ya wananchi na kwa kuyaunga mkono magaidi na makundi ya waasi. Utawala wa Kizayuni unaendelea kufanya mashambulizi ya kijeshi ya moja kwa moja dhidi ya Syria ili kuishughulisha nchi hiyo na mgogoro wa ndani na kuidhoofisha lengo kuu likiwa ni kusogeza mbele stratejia ya nchi za Magharibi ya kutaka kuigawa nchi hiyo ya Kiarabu. Hata hivyo, ukweli ni kuwa, Syria imevuka kipindi hicho na sasa imeingia katika awamu ya kukomboa ardhi za nchi hiyo zilizovamiwa na kukaliwa kwa mabavu. Oparesheni ya kuyakomboa maeneo ya kusini mwa Syria kutoka mikononi mwa magaidi karibu miezi mitatu na nusu iliyopita ambayo imejumuisha mikoa ya Deraa, Qunaitra na Suweyda ni sehemu ya stratijia ya sasa ya serikali ya Syria. Stratejia ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ililenga kukwamisha jitihada za Syria na waitifaki wake za kuwafurusha na kuwangamiza kikamilifu magaidi katika mikoa hiyo. Hii  ni kwa sababu mkoa wa Qunaitra ni sehemu ya eneo la miinuko ya Golan na utawala wa Kizayuni na Marekani zimekuwa zikifanya  jitihada kubwa za kutaka kuliunganisha eneo hilo na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel. 

Eneo la mkoa wa Qunaitra nchini Syria ulio na umuhimu wa kisiasa na kijiografia

Gazeti la Jerusalem Post la Israel mwaka jana liliandika kuwa: Kwa kuzingatia lengo la Israel la kutaka kuigawa vipande vipande nchi ya Syria sasa umewadia wakati wa kuilazimisha jamii ya kimataifa ikubaliane na suala la kuunganishwa miinuko ya Golan na ardhi ya Israel (Palestina inayokaliwa kwa mabavu)

Hata hivyo harakati hizo zimekuwa zikilaaniwa na kukosolewa katika uga wa kimataifa na hapana shaka kwamba, kupasishwa kwa kura nyingi azimio jipya na Umoja wa Mataifa lililosisitiza kuwa Golan ni milki ya Syria ni ujumbe wa wazi kwa Israel kwamba, kukaliwa kwa mabavu eneo hilo ni kitendo kinachopingwa na jamii ya kimataifa na maazimio mengi ya Umoja wa Mataifa likiwemo azimio nambari 497. 

Maoni