Dec 09, 2018 02:52 UTC
  • Jitihada za Marekani za kuzuia maendeleo ya teknolojia ya China

Tangu alipochukua madaraka, Rais Donald Trump wa Marekani ameisababishia China changamoto mbalimbali. China inahesabiwa kuwa nguvu kubwa zaidi ya pili ya kiuchumi duniani.

Hivi sasa kunashuhudiwa hitilafu kubwa kati ya Marekani na China katika nyanja za kisiasa, kibiashara, kiuchumi, kijeshi, kiusalama na kistratejia. Washington imeitaja China kuwa mpinzani wake mkubwa zaidi na amesisitiza udharura wa kukabilia na siasa za nchi hiyo.

Katika upande mwingine, China ni miongoni mwa wapinzani wakubwa wa sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Rais Donald Trump wa Marekani kuhusiana na masuala mbalimbali ya kimataifa na vilevile sera za kiuchumi za serikali ya Washington. Vilevile siasa za Trump za kuzidisha ushuru wa forodha  zimeibua vita vikubwa vya kibiashara kati ya nchi hizo mbili. Japokuwa baada ya mazungumzo ya viongozi wa Marekani na China pambizoni mwa kikao cha wakuu wa kundi la G-20 huko Argentina kulifikiwa mapatano ya kibiashara ya siku 90 baina ya nchi mbili, lakini matukio ya karibuni yanaonyesha kuwa Washington si tu kuwa haina azma ya kufikia mapatano na Beijing bali inataka kuzuia ustawi na maendeleo ya teknolojia ya China. Katika uwanja huo polisi ya Canada imemtia mbaroni Meng Wanzhou ambaye ni Mkurugenzi wa Masuala ya Fedha wa kampuni ya Huawei kutokana na maombi ya Marekani kwa kisingizio kwamba, anakabiliwa na tuhuma za kukiuka vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran. Canada imesema ina mpango wa kumpeleka mkurugenzi  Marekani. Meng Wanzhou mbali na kuwa ni Mkurugenzi wa Masuala ya Fedha wa kampuni ya Huawei ni binti ya mwasisi wa kampuni hiyo na ushahidi unaonesha kuwa, anatarajiwa kuwa mrithi wa baba yake kwenye kampuni hiyo katika siku za usoni. Hatua hiyo imekabiliwa na upinzani mkali wa China na Beijing imetaka kuachiwa huru haraka iwezekanavyo Meng Wanzhou. 

Meng Wanzhou, Mkurugenzi wa kampuni ya Huawei aliyekamatwa Canada kwa agizo la Marekani 

Wakati huo huo Russia pia imeunga mkono msimamo wa China. Kuhusiana na suala hili Sergey Lavrov Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa: Kutiwa mbaroni nchini Canada Meng Wanzhou mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Huawei kwa ombi la Marekani ni mfano wa utumiaji wa sheria za ndani katika masuala ya kimataifa na hatua hii ya Marekani imezikasirisha nchi nyingi. Kinyume chake, Washington imeiunga mkono Canada. Kuhusiana na suala hilo, Larry Kudlow Mkurugenzi wa Baraza la Uchumi la Taifa la Marekani anasema: Tuliitahadharisha Huawei kitambo nyuma kuhusu ukiukaji wa vikwazo dhidi ya Iran. 

Ingawa kisingizio kinachotumiwa na Marekani kuhalalisha hatua hiyo ni madai kwamba, Huawei imekiuka vikwazo vya Washington dhidi ya Iran, lakini ukweli wa mambo ni zaidi ya kadhia hii. Kampuni ya Huawei hivi sasa inahesabiwa kuwa miongoni mwa makampuni yanayoongoza dunia katika teknolojia ya mawasiliano na simu za rununu na imepanua sana shughuli zake ulimwenguni kote. Marekani inadai kuwa, kampuni ya Huawei imeiba teknolojia. Mwaka 2007 kampuni hiyo ilikuwa na mpango wa kununua kampuni moja iliyoko Washington ambayo ilikuwa ikijihusisha na uzalishaji wa zana za mawasiliano ya mtandao. Hata hivyo viongozi wa Marekani walikwamisha muamala huo. Mwaka 2011 pia viongozi wa Marekani walifuta mkataba wa dola bilioni mbili wa kampuni ya Huawei kwa ajili ya kununua sava (Server) kutoka kampuni moja ya Kimarekani. Wachina waamini kwamba, sababu kuu iliyoifanya Marekani iituhumu kampuni ya Huawei kuwa inafanya ujasusi ni kutaka kulinda maslahi ya makampuni ya Kimarekani na kuzuia bidhaa za Huawei kuenea katika soko la ndani la Marekani. Bidhaa zinazozalishwa na kampuni ya Huawei zinatambulika kuwa nembo ya nguvu ya Wachina katika masoko ya kimataifa. Katika miaka ya karibuni Huawei ilikuwa na karibu asilimia 13 katika masoko ya simu erevu (smart phones) huku kampuni ya Apple ya Marekani ikiwa na asilimia 12 ya soko la bidhaa hiyo. Kwa msingi huo, makampuni hayo mawili ya Apple na Huawei yanashindana vikali kushika nafasi ya pili katika uuzaji mkubwa zaidi wa simu za mkononi (Rununu). Aidha utumiaji wa suhula za simu na mawasiliano za kampuni hiyo vimeibua wasiwasi wa kiusalama nchini Marekani katika miaka ya karibuni na serikali za Obama na Trump zilizitaka nchi za Ulaya zipunguza kiwango cha utumiaji wa bidhaa za Huawei.

Marekani sasa inatumia kisingizio cha kukiukwa vikwazo dhidi ya Iran kuisumbua na kuibana kampuni ya Huawei lakini ukweli wa mambo ni kuwa, Washington imechukua hatua hiyo ili kubana uwepo wa kampuni hiyo nchini Marekani na wakati huo iweze kuwashawishi waitifaki wake wa Ulaya ili wachukue hatua sawa na hiyo dhidi ya Huawei. Na kwa msingi huo imetaka kupelekwa Marekani Meng Wanzhou, Mkurugenzi wa Masuala ya Fedha wa Kampuni hiyo. Tunaweza kutabiri kuwa kutekelezwa kivitendo jambo hili kutakabiliwa na jibu kali la serikali ya China na kuzidisha mivutano kati ya pande mbili.   

Tags

Maoni