Dec 12, 2018 12:32 UTC
  • China yarudisha mapigo, yapiga marufuku simu za iPhone

Kampuni ya Apple ya Marekani imepata pigo kubwa baada ya mahakama moja ya China kupiga marufuku uuzaji wa simu za iPhone nchini Uchina.

Hatua hiyo ni matokeo ya kesi iliyowasilishwa mahakamani mwishoni mwa mwaka jana na kampuni ya Qualcomm dhidi ya Apple ikiituhumu kuwa imeiba teknolojia yake. Kwa mujibu wa uamuzi wa mahakama hiyo, simu zote za rununu za iPhone zilizozalishwa kuanzia mwaka 2015 hadi iPhone X zimepigwa marufuku kuuzwa nchini China. Hii ni licha ya kwamba, China inahesabiwa kuwa miongoni mwa masoko makubwa zaidi la simu za rununu za iPhone duniani.

Ripoti zinasema hisa za kampuni ya Apple ya Marekani zilishuka chini kwa asilimia 2 mapema siku ya Jumatatu.

Hukumu hiyo ya Mahakama ya China imetolewa wakati dunia ikiendelea kushuhudia vita kali ya kibiashara baina ya Marekani na China. Uamuzi huo pia umechukuliwa baada ya Marekani kuiomba Canada impeleke Washington Mkurugenzi wa Masuala ya Fedha wa kampuni ya teknolojia ya mawasiliano ya Huawei, Meng Wanzhou anayezuiliwa nchini humo kwa kisingizio cha kukiuka vikwazo vya Marekani.

Meng Wanzhou

Wanzhou alikamatwa Disemba Mosi kufuatia ombi la Marekani wakati akiwa katika uwanja wa ndege mjini Vancouver, Canada. Meng ambaye ni bintiye mwanzilishi na mmiliki wa kampuni ya Huawei, Ren Zhengfei, anatajwa kuwa mrithi mtarajiwa wa msimamizi wa shirika hilo. Alikamatwa kwa tuhuma kuwa shirika la Huawei, kupitia shirika lingine, limekiuka vikwazo vya Marekani kwa kuiuzia Iran vifaa vya mawasiliano.

Mapema leo Canada imemwachia huru Meng Wanzhou kwa dhamana. China imeitahadharisha Canada isimkabidhi kwa Marekani la sivyo itakabiliwa na hatua kali.   

Tags

Maoni