Dec 12, 2018 16:19 UTC
  • Trump atishia kutokea machafuko Marekani iwapo ataitwa kujieleza

Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kuwa nchi hiyo itakumbwa na machafuko iwapo ataitwa kujieleza.

Ametoa vitisho hivyo wakati alipohojiwa na shirika la habari la Reuters na kusema: "Ni vigumu kumwita kujieleza mtu ambaye hajafanya kosa lolote na ambaye anajenga uchumi bora katika historia ya nchi yetu."

Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kuitwa kujieleza mbele ya Baraza la Congress, Trump amedai kuwa hashughulishwi na jambo hilo na kwamba anadhani watu watafanya fujo kama hilo litatokea.

Trump amedai kuwa hashughulishwi na jambo hilo wakati ripoti mbalimbali zinaonesha jinsi rais huyo wa Marekani alivyo na wasiwasi mkubwa kuhusu kampeni ya kumtaka ajieleze kuhusiana na ushirikiano wake na Russia.

Rais wa Marekani anatuhumiwa na shutuma nyingi za kila upande hasa za uasherati

Televisheni ya CNN iliripoti siku ya Jumatatu ikinukuu duru moja ya Ikulu ya Marekani, White House ambayo haikutaka kutajwa jina ikisema kwamba, Trump anahisi kuna uwezekano mkubwa wa yeye kuitwa na kujieleza katika wakati huu ambapo chama cha Democrat kina viti vingi katika bunge la Marekani.

Uchunguzi kuhusu ushirikiano wa Trump na Russia ambao unaoongozwa na mkuu wa taasisi huru ya uchunguzi, Robert Mueller uligonga vichwa vya habari siku ya Ijumaa baada ya mahakama kufichua kwamba, wakili wa zamani wa Trump, Michael Cohen amempa Mueller taarifa muhimu za kumsaidia katika uchunguzi wake.

Mbali na tuhuma za kushirikiana na Russia, Trump ana kesi nyingine nyingi za kujibu hasa za uasherati na ufisadi wa kimaadili.

Maoni