Dec 13, 2018 02:28 UTC
  • Marekani yachukua mateka katika vita vyake vya kibiashara na China

Baada ya Donald Trump kuingia madarakani kama rais wa Marekani Januari mwaka 2017, amekuwa akifuatilia sera hasimu na zenye utata kuhusu China na hivyo kuwaibulia wakuu wa China changamoto kadhaa. Moja ya sera ambazo Trump ametekeleza ni kuongeza ushuru wa forodha kwa bidhaa kutoka China na kwa njia hiyo kutangaza rasmi vita vya kibiashara dhidi ya China.

Pamoja na kuwa baada ya mazungumzo ya hivi karibuni baina ya Rais Xi Jinping  wa China na Donald Trump pembizoni mwa mkutano wa G20 nchini Argentina, nchi mbili zilitangaza usitishaji vita vya kibiashara kwa muda wa siku 90, lakini matukio ya hivi karibuni yameonyesha kuwa si tu kuwa Marekani haitaki suluhu na China bali pia haitaki kuona China inaongoza katika uga wa teknolojia duniani.

Katika tukio muhimu, mnamo Disemba Mosi, kufuatia ombi la Marekani, Canada ilimkamata Bi. Meng Wanzhou Mkurugenzi wa Masuala ya Fedha katika Shirika la Huawei  ambaye alikuwa katika Uwanja wa Ndege wa Vancouver akielekea nyumbani. Anatuhumiwa kuwa amekiuka vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya Iran na sasa Marekani inataka kumfikisha katika mahakama zake ajibu mashtaka. 

Siku chache zilizopita Serikali ya China ilitoa onyo kali na kuitaka Canada imuachie huru mara moja mkuu huyo wa Huawei na isithubutu kumkabidhi kwa wakuu wa mahakama za Marekani.  China iliitaka pia Canada ihakikishe haki zake za kisheria zinalindwa la sivyo Canada itabeba dhima ya matokeo mabaya ya kadhia hiyo. Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amedai kuwa hakuna malengo yoyote ya kisiasa katika kukamatwa Wanzhou ambaye pia ni bintiye mwanzilishi wa shirika la Huawei. Hatimaye Jumanne hii, kufuatia indhari hiyo ya China,  mahakama ya Canada ilimuachilia huru Wanzhou kwa dhamana ya dola milioni 10.

Trump

Rais Trump ameashiria uamuzi wa kumuachilia huru afisa huyo wa ngazi za juu wa Shirika la Huawei na kusema: "Yumkini kuachiliwa mkurugenzi wa masuala ya fedha katika Shirika la Huawei kukawa sehemu ya mapatano makubwa ya kibiashara na China." Tamko hilo la Trump linaonyesha kuwa, kwa mtazamo wake, kuachuliwa huru afisa huyo wa ngazi za juu wa Huawei ni sehemu na muafaka mkubwa na China na hivyo yamkini Marekani hapo ikafaidika pakubwa kutoka China.

Hii ni katika hali ambayo wakuu wa Marekani wamekuwa wakijaribu kuonyesha kuwa kadhia ya mkurugenzi huyo wa Huawei haina uhusiano wowote na msuguano wa kibiashara na China. 

Kuhusiana na hili, Larry Kudlow Mkurugenzi wa Baraza la Kitaifa la Uchumi Marekani alikuwa amesema: "Kadhia ya kukamatwa afisa wa Huawei haina uhusiano na mazungumzo ya kibiashara na China.

Hivi sasa kwa matamshi ya Trump, imebainika wazi kuwa kukamatwa Mkurugenzi wa Masuala ya Fedha katika Shirika la Huawei kulikuwa ni sehemu ya mchezo wa karata wa wakuu wa Marekani katika mazungumzo yajayo na China na ilikuwa ni njia ya kuishinikza zaidi China.

Pamoja na hayo, uzoefu kuhusu vita vya kibiashara kati ya China na Marekani katika miezi ya hivi karibuni unaonyesha kuwa, Wachina wamekuwa wakitoa jibu kwa kila hatua ya kihasama inayochukuliwa na Marekani na hivyo kuwalazimu wakuu wa Washington kulegeza msimamo.

Katika upande wa pili kukamatwa Wanzouh kunaonyesha kuwa Shirika la Huawei sasa litakumbwa na hali ngumu katika shughuli zake katika eneo la Amerika Kaskazini. Kati ya hatua ambazo Marekani inaweza kuchukua kuliadhibu Shirika la Huawei ni kuliwekea shirika hilo vizingti  katika kufanya kazi Marekani au kulitimua kabisa nchini humo.

Lakini iwapo Canada itaikabidhi Marekani mkurugenzi huyo wa Huawei na kisha achukuliwe hatua kali hasa kufungwa jela kwa muda mrefu, basi itathibiti kuwa kadhia hiyo ni kubwa zaidi ya kisingizio cha kukiuka vikwazo dhidi ya Iran.

Marekani imekuwa ikiwataka washirika wake barani Ulaya na Asia Mashariki wasitishe ushirikiano na Shirika la Huawei. Mashinikizo hayo yamekuwa na mafanikio kwa kiasi fulani kwani baadhi ya nchi zimetii matakwa ya Washington na kuliwekea shirika hilo vizingiti. Kwa maelezo hayo, kukamatwa mkuu wa masuala ya kifedha katika Shirika la Huawei kwa sababu ya kukiuka vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni kisingizio tu kwani lengo kuu la watawala wa Washignton ni kulibana shirika hilo ili kuzuia kuenea satwa ya kiteknolojia ya China duniani na hivyo kuilazimisha China ilegeze msimamo katika vita vyake vya kibiashara na Marekani.

Tags

Maoni