Dec 14, 2018 02:42 UTC
  • Msimamo makini wa Russia, wa kupinga JCPOA kuhusishwa na masuala mengine ya Iran

Baada ya Marekani kujitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mnamo mwezi Mei mwaka huu wa 2018, kila mara imekuwa ikijaribu kufanya kila njia kuzishusisha shughuli za nyuklia za Iran na masuala mengine, ili kutetea na kuhalalisha uamuzi wake wa kujitoa kwenye makubaliano hayo.

Katika mwendelezo wa hila hiyo, Washington imekuwa ikilikuza suala la mpango wa makombora wa Iran, sambamba na kuonyesha kuwa sera na hatua za Jamhuri ya Kiislamu katika eneo ni hatari na tishio ili kupata uungaji mkono wa wanachama waliosalia wa JCPOA wa kundi la 4+1 katika kuchukua msimamo dhidi ya Tehran.

Hata hivyo msimamo huo wa Marekani umekuwa ukipingwa kila mara na kundi hilo hususan mrengo wa nchi za Mashariki, yaani Russia na China. Katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika siku ya Jumatano ya tarehe 12 Desemba kujadili ripoti ya Katibu Mkuu wa umoja huo kuhusu utekelezwaji wa azimio nambari 2231, balozi na mwakilishi wa Russia UN, Vasily Nebenzya alisisitiza kwamba, Moscow inapinga kuyahusisha makubaliano ya nyuklia ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA na masuala mengine. Kwa mujibu wa Nebenzya: Russia inaheshimu na kutekeleza mwito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kulindwa JCPOA, ambayo ni makubaliano yenye umuhimu wa kimsingi kwa amani ya eneo na ya kimataifa; na inakubaliana na mtazamo kwamba, masuala ambayo hayamo kwenye makubaliano hayo yasitumiwe kuwa kisingizio cha kuvunja JCPOA. 

Vasily Nebenzya, balozi na mwakilishi wa Russia UN

Kwa mtazamo wa Moscow, hivi sasa kuna hali ya mgongano kuhusiana na makubaliano ya JCPOA, kwa sababu Marekani, ambayo ni mmoja wa wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, si tu inakaidi dhahiri shahiri kutekeleza azimio nambari 2231 la baraza hilo, lakini pia inataka kuziadhibu nchi nyingine wanachama, kwa sababu ya kutekeleza maamuzi ya Baraza la Usalama na Tume ya Pamoja ya JCPOA. Msimamo huo wa Russia unapingana waziwazi na msimamo wa Marekani. Katika kikao cha karibuni cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo alidai kwamba, shughuli za makombora ya balestiki ya Iran zimetoka nje ya udhibiti. Kwa kudai kwamba Iran inatumia njia na mbinu tofauti kukwepa kutekeleza azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama, Pompeo ametaka majaribio ya makombora ya Iran yakomeshwe. Hata hivyo, na kama alivyoeleza bayana balozi wa Russia katika Umoja wa Mataifa, hakuna uhusiano wowote kati ya JCPOA na mpango wa makombora wa Iran. Marekani, kama ilivyokuwa hapo kabla, yaani yalipotangazwa masharti 12 ya Pompeo kuhusu Iran, imekuwa ikidai kila mara kwamba, kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya mpango wa nyuklia wa Iran na masuala mengine, hususan mpango wa makombora na sera za kieneo za Iran.

Mike Pompeo (katikati) katika kikao cha UNSC

Mtazamo na muelekeo huo wa Washington, haukubaliwi na wanachama wengine wa JCPOA na Umoja wa Mataifa, kwa sababu matakwa ya Marekani yanavuka mpaka wa masuala ya nyuklia kama yalivyobainishwa kwenye makubaliano ya JCPOA. Inachotaka hasa Marekani ni kufungwa kikamilifu shughuli za nyuklia za Iran, kusimamisha moja kwa moja mipango yake ya makombora na kuachana Tehran na sera na hatua inazochukua kuhusiana na nchi za eneo hili. Matakwa hayo ya Marekani yamepingwa vikao na Iran, ambayo sambamba na kusisitiza kwamba, itaendelea kutekeleza makubaliano ya JCPOA, tab'an kwa sharti la kudhamini maslahi yake, haikubaliani abadani na mtazamo wa kuuwekea mpaka na vizuizi mpango wake wa makombora na sera zake katika eneo.

Makombora ya masafa marefu ya Iran yanayoitia kiwewe Marekani na utawala wa Kizayuni

Japokuwa Pompeo amedai kwamba Marekani inataka kushirikiana na nchi zote wanachama wa Baraza la Usalama ili kuchukua hatua kali zaidi za kuubana mpango wa makombora ya balestiki wa Iran kupitia Umoja wa Mataifa, hata hivyo yeye mwenyewe anaelewa fika kwamba, hakuna uwezekano wowote wa Washington kufanikisha takwa lake hilo. Ni kama alivyoeleza Barbara Slavin, mtaalamu wa masuala ya kisiasa kwamba: Hotuba ya Pompeo katika kikao cha Baraza la Usalama, ni maneno matupu ya porojo yanayolenga kuendesha vita vya habari na vya kisaikoljia. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halitachukua hatua dhidi ya mpango wa makombora ya balestiki ya Iran. Maudhui hiyo ilishatajwa hapo kabla katika azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama; na Iran ikasisitiza kuwa majaribio yake hayajakiuka azimio hilo.

Inavyoonyesha, sera za Marekani kuhusiana na JCPOA, ambazo zinafuata muelekeo wa sera zingine za nchi hiyo, za uchukuaji hatua za upande mmoja, hazina nafasi yoyote ya kufanikiwa. Na kwa kuzingatia hali halisi tunaweza kutabiri kuwa, hatimaye Washington italazimika kukiri kwamba sera zake hizo zimegonga mwamba.../

Tags

Maoni