Dec 14, 2018 04:27 UTC
  • Pigo jingine kwa Trump, Baraza la Senate la Marekani lapasisha maazimio dhidi ya Saudia

Licha ya rais wa Marekani, Donald Trump kumkingia kifua sana Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, lakini Baraza la Senate la nchi hiyo limepasisha maazimio mawili yaliyo dhidi ya Saudia.

Azimio la kwanza lililopasishwa na Baraza la Senate la Marekani ni la kukomesha uungaji mkono wa kijeshi wa nchi hiyo kwa vita vya Saudi Arabia dhidi ya Yemen na la pili ni la kumtambua rasmi Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia kuwa muhusika wa mauaji ya kikatili na ya kinyama ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo mapema leo alfajiri na kuongeza kuwa, miswada ya maazimio hayo imewasilishwa mbele ya Baraza la Sanate la Marekani na Bernie Sanders, seneta wa kujitegemea wa jimbo la Vermont na Mike Lee, seneta wa chama cha Trump cha Republican kutoka jimbo la Utah.

Baraza la Senate la Marekani lapasisha maazimio mawili dhidi ya Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia.

 

Maazimio hayo yamepasishwa katika hali ambayo rais wa Marekani anapinga vikali kukatwa uungaji mkono wa nchi hiyo kwa Saudi Arabia.

Katika upande mwingine, seneta mwingine wa chama cha Republican, Bob Corker wa jimbo la Tennessee ambaye pia ni mkuu wa kamati ya uhusiano wa mambo ya nje ya Baraza la Senate la Marekani amewasilisha muswada wa azimio jingine ambalo ndani yake, Mohammad bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia anatajwa kuwa ndiye muhusika mkuu wa mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo wa mjini Istanbul, Uturuki.

Maoni