Dec 14, 2018 15:52 UTC
  • Trump kuwa mwenyeji wa Bin Salman na Netanyahu katika 'Camp David ya 2'

Gazeti la Middle East Eye limeripoti kuwa, Mohammad Bin Salman Aal Saud, Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia anatafakari sana juu ya kufanya mkutano na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu chini ya upatanishi na uenyeji wa Rais Donald Trump wa Marekani.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, mkutano huo wa Netanyahu na Bin Salman unatazamiwa kushabihiana na ule uliopelekea kusainiwa makubaliano ya Camp David.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa, Mkataba wa Camp David ni makubaliano ya kwanza ya suluhu tangu baada ya vita vya Waarabu na Israel yaliyosainiwa mwaka 1978 katika enzi za utawala wa Rais Anwar Sadat nchini Misri na kupelekea kuanzishwa uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia baina ya Misri na utawala haramu wa Kizayuni, 

Duru za habari zimefichua kuwa, kadhia hiyo ya Netanyahu na Bin Salman kufanya mkutano na kupeana mikono imezusha mgogoro na mpasuko mkubwa miongoni mwa maafisa wa ngazi za juu ndani ya utawala wa Aal-Saud waliopewa jukumu la kuandaa mazingira ya kikao hicho, wakiwemo washauri wa kisiasa, waandishi wa habari na maofisa kutoka idara za kiintelijensia, jeshi na Wizara ya Mambo ya Nje.

Netanyahu na Rais wa Misri, Muhammad al-Sisi

Haya yanaarifiwa siku chache baada ya kanali mashuhuri ya televisheni ya Hadashot ya utawala haramu wa Israel kufichua kuwa, Tel Aviv ipo mbioni kuwa na uhusiano wa kidiplomasia na Saudi Arabia, na kwamba uhusiano wa tawala mbili hizo utafanywa wa kawaida na rasmi ndani ya miezi michache ijayo.

Katika miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko la mikutano ya siri na ya dhahiri baina ya viongozi na maafisa wa ngazi za juu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia katika fremu ya kuandaa uhusiano wa kawaida baina ya pande mbili.

Tags

Maoni