Dec 15, 2018 02:39 UTC
  • Serikali ya Afghanistan; mwakilishi pekee kisheria wa kufanya mazungumzo na Taliban

Naibu msemaji wa Rais wa Afghanistan amesema, timu ya mazungumzo kutoka serikalini ndiyo pekee iliyo na ustahiki wa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na kundi la Taliban.

Aref S'amim, ameyasema hayo katika radiamali na mjibizo aliotoa kwa hatua ya vyama vya siasa vya nchi hiyo ya kuunda timu ya wawakilishi wao katika mazungumzo na Taliban; na akaongezea kuwa, ujumbe wa mazungumzo wa serikali ndio unaopaswa kufanya mazungumzo na kundi hilo. Hivi karibuni, serikali ya Afghanistan iliunda jopo la watu 12 kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya amani na kundi la Taliban, hatua ambayo imechochea malalamiko na upinzani wa vyama na Baraza Kuu la Suluhu la nchi hiyo.

Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan

Hata kama serikali ya Afghanistan imeunda pia tume ya ushauri itakayotoa ushauri kwa jopo litakalofanya mazungumzo na kundi la Taliban, lakini vyama vya siasa vina wasiwasi kwamba, maoni na mitazamo yao hayatozingatiwa katika mazungumzo na Taliban. Kwa mtazamo wa wafuatiliaji wa siasa za Afghanistan, kutolewa mitazamo inayotafautiana na kufanywa juhudi tofauti za kisiasa na kimirengo kwa ajili ya kufanya mazungumzo na kundi la Taliban kunatokana na udhaifu wa serikali ya Kabul katika kuratibu na kuongoza mchakato huo.

Hivi karibuni, na baada ya harakati zilizoanzishwa na Zalmay Khalilzad, mwakilishi wa Marekani katika masuala ya Afghanistan, katika mchakato wa kutafuta suluhu ya nchi hiyo, sambamba na hatua yake ya kujaribu kushika hatamu za mwelekeo wa mchakato huo, Rais Muhammad Ashraf Ghani, naye pia ameamua kujitutumua na kuunda timu maalumu ili kuhakikisha hatamu za kusimamia mchakato wa amani ya Afghanistan zinabaki mikononi mwa serikali ya Kabul.

Zalmay Khalilzad

Fadhlurahman Urya, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema:

"Katika siku za karibuni, zimepigwa hatua nzuri kwa ajili kuleta suluhu na amani Afghanistan. Kwa kuzingatia fursa na uwezo ilionao serikali, endapo muundo wa Baraza Kuu la Suluhu utaimarishwa, tunaweza kutoa tathmini kwamba, mchakato wa amani wa nchi hiyo una muelekeo chanya. Hakuna shaka yoyote kwamba, ikiwa serikali itashauriana na itakuwa na uratibu kamili na Baraza Kuu la Suluhu kwa ajili ya kuleta amani, baada ya muda, matokeo mazuri yatapatikana."

Kwa kuzingatia taarifa zilizopo, kwamba serikali ya Afghanistan na Marekani zimedhamiria kuukamilisha mchakato wa amani ya Afghanistan kabla ya uchaguzi ujao wa rais wa nchi hiyo, vyama na makundi ya kisiasa, nayo pia yanataka yashirikishwe kwenye mchakato huo na yameeleza bayana kwamba, yanapinga hatua ya serikali ya kuwashirikisha kiupendeleo katika suala hilo viongozi wa vyama vya siasa vya nchi hiyo.

Wanamgambo wa kundi la Taliban

Viongozi wa vyama na makundi ya kisiasa nchini Afghanistan yanaitakidi kuwa, badala ya rais wa nchi hiyo kulipa nguvu Baraza Kuu la Suluhu, ambalo linajumuisha wawakilishi wa mirengo yote ya kisiasa, kikabila na kidini ili kusukuma mbele gurudumu la mchakato wa amani, ameunda vikundi maalumu vya kufanya mazungumzo na Taliban, hatua ambayo ni sawa na kukabidhi kazi moja kwa watu wawili tofauti; na hasa yakizingatiwa malengo na mipango inayotekelezwa na Baraza Kuu la Suluhu la nchi hiyo. 

Alaa kulli haal, inavyoonyesha, viongozi wa makundi na vyama vya siasa nchini Afghanistan wanahisi kwamba, Ashraf Ghani, ambaye hajapata mafanikio maalumu wala mtaji wowote wa kisiasa kwa ajili ya kuwania tena urais katika uchaguzi ujao, anataka iwe iwavyo ahakikishe anafanya mapatano na kufikia mwafaka na kundi la Taliban, hata kama ni kwa gharama ya kuifanyia mabadiliko katiba kwa ajili ya kuridhia matakwa na utashi wa kundi hilo. Na hii ni pamoja na kuwa, kwa mtazamo wa vyama vya siasa, suluhu na amani ya Afghanistan ni suala ujumuishi kamili wa kitaifa; na kuhusu vipengele vya mwafaka na namna ya kuuratibu mwafaka wenyewe, inapasa mirengo yote ya kisiasa, kikabila na kidini ikubaliane na kuwa na kauli moja juu ya suala hilo; na Baraza Kuu la Suluhu ndiyo marejeo makuu yenye ustahiki wa kusimamia jambo hilo ilhali serikali inataka kulidhoofisha baraza hilo.

Hivi sasa kuna wasiwasi nchini Afghanistan kwamba, kwa hatua yake ya kumkabidhi mkuu wa ofisi yake uongozi wa jopo maalumu la kufanya mazungumzo na kundi la Taliban, Rais Ashraf Ghani, si tu ameingilia moja kwa moja mazungumzo hayo, lakini anaweza pia akatoa ahadi hizi na zile kwa kundi hilo, ambazo yamkini katika siku za usoni zitakuja kusababisha madhara kwa maslahi, mamlaka ya utawala, umoja na mshikamano wa kitaifa wa Afghanistan.../

Tags

Maoni