Dec 16, 2018 07:42 UTC
  • Uingereza yailaumu Israel kwa kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

Msemaji wa serikali ya Uingereza ameilaumu Israel kwa kuendeleza ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi inazowapora Wapalestina.

Edwin Samuel ambaye ni msemaji wa serikali ya Uingereza katika masuala ya Magharibi mwa Asia na Afrika Kaskazini alisema hayo jana wakati alipohojiwa na televisheni ya Palestina na kusisitiza kuwa, ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni jambo lililo kinyume cha sheria na kwamba serikali ya Uingereza inalihesabu suala hilo kuwa ni sehemu ya ukaliaji kwa mabavu ardhi za watu wengine.

Amesema, Uingereza kamwe haitolinyamazia kimya jambo hilo na itatumia kila fursa inayojitokeza kuishawishi Israel iache kuvunja sheria za kimataifa.

Maandamano ya kupinga Uzayuni

 

Msemaji huyo wa serikali ya Uingereza vile vile amesema kuhusu tathmini ya nchi yake juu ya kuongezeka mivutano ya kisiasa na kijeshi ya utawala wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan kwamba, London inafanya juhudi kubwa za kisiasa na kidiplomasia hasa ndani ya Umoja wa Mataifa kuhakikisha kuwa maazimio yote ya umoja huo na ya Baraza la Usalama yanaheshimiwa kuhusu nchi huru ya Palestina.

Msimamo huo wa msemaji wa serikali ya Uingereza wa kuliunga mkono taifa la Palestina umetokana na mashinikizo ya makundi ya haki za binadamu yanayoliunga mkono taifa hilo linalodhulumiwa kila upande.

Tags

Maoni