Dec 18, 2018 03:24 UTC
  • Mustakabali usiojulikana kuhusu maandamano ya wananchi Ufaransa

Maandamano nchini Ufaransa yangali yanaendelea hata baada ya Rais Emmanuel Macron kulegeza msimamo na kukubali kupunguza ushuru wa petroli na kufanyika marekebisho ya sheria zinazohusu kustaafu wafanyakazi wa umma. Édouard Charles Philippe Waziri Mkuu wa Ufaransa amekiri kuwa serikali imefanya kosa katika kukabiliana na vugugu la wananchi wanaoandamana na haijawasikiza kama ilivyopaswa.

Kauli ya Waziri Mkuu wa Ufaransa inakuja wakati ambao maandamano yangali yanaendelea kote Ufaransa. Maandamano ya wananchi wa Ufaransa ambao yamepewa jina la "Harakati ya Vizibao vya Njano" sasa yameingia wiki ya saba. Hii ni katika hali ambayo wakuu wa nchi hiyo walikuwa na matumaini kuwa, ahadi alizotoa Macron zingewafanya waandamanaji walegeze misimamo na kumpa rais fursa ya kutekeleza mpango wake.

Malengo ya maandamano hayo sasa yamebadilika kutoka masuala ya kiuchumi na sasa waandamanaji wanataka kufanyike kura ya maoni na pia Macron aondoke madarakani.

Herve Le Bras mtaalamu wa masuala ya jamii wa Ufaransa anatahadharisha kuhusu hali ya mambo nchini humo na kusema: "Yumkini maandamano ya wananchi yamepungua kiasi lakini inaelekea kuwa, idadi kubwa ya waandamanaji wanamlenga Macron na wanataka ajiuzulu."

Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema Macron atahitajia bajeti ziada ya zaidi ya Euro bilioni 10 kutekeleza ahadi alizotoa kwa waandamanaji. Ni kwa msingi huo ndio maana weledi wa mambo ya kiuchumi wakasema kuwa, kusitisha mpango wa marekebisho ya kiuchumi na kutekelezwa mpango wa ruzuku kama alivyoahidi Macron ni jambo lisilowezekana. Bunge la Ufaransa limesema iwapo hatua ambazo serikali imependekeza kwa ajili ya kuzima maandamano ya wanaopinga mfumo wa ubepari Ufaransa zitatekelezwa basi nchi hiyo itakumbwa na nakisi ya bajeti.

Rais Macron

Uchumi wa Ufaransa umekuwa ukilegalega hasa kabla ya mwaka 2008 wakati bara zima la Ulaya lilipokumbwa na matatizo ya kiuchumi. Ingawa marais waliotangualia wa Ufaransa walijaribu kuboresha hali ya kiuchumi nchini humo lakini hawakuweza kunusuru uchumi wa nchi hiyo. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, chimbuko la matatizo ya hivi sasa ya Ufaransa ni sera za marekebisho ya kiuchumi ambazo zilitekelezwa na Francois Hollande.

Japokuwa maandamano ya 'Vuguvugu la Visibao Vya Njano' yanasemekana kuwa yametokana na sera za kiuchumi za Macron lakini ukweli ni kuwa, hali ya kisiasa na kijamii ya Ufaransa inaoonyesha kuwa maandamano hayo yametokana na matatizo ya kimsingi ya kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini humo.

Aghalabu ya waandamanaji wanalalamikia ukosefu wa uadilifu  katika jamii ya Ufaransa na wanataka kufanyike kura ya maoni kubadilisha hali ya sasa ambayo inawanufaisha mabepari waliowachache.

Quentin Delurmoz, mwanashistoria wa Ufaransa anasema: Maandamano dhidi ya mfumo wa ubepari nchini humo ni ishara ya mgogoro wa kijamii na kisiasa katika mfumo wa demokrasia nchini humo.

Rais wa zamani wa Ufaransa Francois Hollande

Mgogoro wa Ufaransa unaendelea, na wakuu wa nchi hiyo wana wasiwasi kuhusu mustakabali. Si tu kuwa viongozi hao wamelegeza misimamo ili kujaribu kutuliza maandamano bali hata wametoa ahadi za kuboresha hali ya mambo. Pamoja na hayo inaonekana kuwa waandamanaji hawajaridhika na ahadi zilizotolewa na wanataka mabadiliko ya kimsingi nchini Ufaransa. Mmoja wa waandamanaji amenukuliwa akisema: "Macron anatuchezea, sisi tuko tayari kuendelea hadi mwisho, tunataka mfumo huu wa Jamhuri usambaratike."

Katika hali kama hii, kadiri muda unavyosonga mbele, itabainika iwapo serikali ya Ufaransa itaweza kukidhi matakwa ya waandamanaji na kupunguza wimbi la hasira au la.

Tags

Maoni