Dec 18, 2018 06:45 UTC
  • Guterres atahadharisha kuhusu vitisho vya mfumo wa kambi kadhaa

Baada ya kusambaratika Urusi ya zamani na kumalizika kipindi cha Vita Baridi hapo mwaka 1991 mfumo wa kambi mbili za Mashariki na Magharibi pia ulitoweka na kumalizika.

Dunia hususan katika miongo miwili iliyopita imekuwa katika hali ya kuondoka katika mfumo wa kambi moja kuelekea mfumo wa kambi kadhaa. Hata hivyo hadi sasa misingi na nguzo za mfumo huo mpya wa kimataifa bado haijathabitishwa, na Marekani ambayo inadai kuwa ni nguvu kubwa zaidi duniani imekuwa ikifanya jitihada za kukwamisha mwenendo huo na kusimika mfumo wa sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja katika mahusiano ya kimataifa (Unilateralism). 

Kilele cha jitihada hizo za Marekani kimeonekana katika kipindi cha uuongozi wa Rais Donald Trump. Kipindi cha uongozi wa Donald Trump kinaweza kutambuliwa kuwa ndio kipindi cha kuhuishwa tena sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja. Chini ya kivuli cha kaulimbiu ya "Marekani Kwanza", na kwa kutanguliza mbele maslahi na malengo ya serikali ya Washington na kupuuza maslahi ya nchi nyingine, Trump anaamini kuwa, sera hizo za kujichukulia maamuzi ya upande zinazidisha nguvu za serikali ya Washington na kuifanya iwashinde na kuwa juu ya wapinzani wake.  

Rais Donald Trump wa Marekani 

Kiongozi huyo wa Marekani amekuwa akitumia mabavu na siasa hizo kwa ajili ya kutimiza malengo yake katika masuala muhimu ya kimataifa. Sera hizo za Trump pia zinasisitiza kuwa, Marekani ni polisi ya dunia na kwamba ndiyo inayopasa kushughulikia masuala yote muhimu ya kimataifa tena kwa kutumia mabavu kama nguvu za kijeshi na uwezo wake wa kiuchumi.

Ukweli ni kwamba, katika kipindi cha sasa ambapo dunia inaelekea kwenye mfumo wa kambi kadhaa, ishara zote zinaonyesha kuwa sera na mwelekeo wa Marekani hauoani wala kwenda sawa na mabadiliko na uhakika wa hali ya kimataifa. Sera hizo pia zinazidisha hali ya kutengwa Marekani katika mahusiano ya kimataifa. Vilevile sisitizo la Trump na msimamo wake wa kung'ang'ania sera na siasa za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja (Unilateralism) zinahatarisha mwelekeo wa sasa wa dunia kwenye mfumo wa kambi kadhaa (Multilateralism) unaotambuliwa kuwa kigezo bora zaidi katika mahusiano ya kimataifa katika zama za sasa.

Katika mkondo huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alisema katika hotuba yake ya Jumapili iliyopita mwishoni mwa mkutano wa kimataifa wa Doha kwamba, kuna udharura wa kuimarishwa ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kukomesha mapigano na mizozo ya aina zote kote duniani. Guterres amesema mfumo wa kambi kadhaa (Multilateralism) na ushirikiano wa kimataifa vinakabiliwa na hatari kubwa.

Katibu Mkuu wa UN katika mkutano wa Doha na Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Aal Thani Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar 
 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa: Kwa sasa mfumo wa kambi kadhaa na ushirikiano wa kimataifa vinakabiliwa na hatari kubwa kuliko wakati wowote mwingine. Guterres anaamini kwamba, kipindi cha kuelekea kwenye mfumo wa kambi kadhaa duniani ni kipindi kinachoandamana na machafuko na ndiyo maana dunia ya sasa inasumbuliwa na vurugu na hali ya mchafukoge.

Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, miongoni mwa sifa za kipindi cha sasa ni kutokea mambo yasiyotabirika, suala ambalo limezidisha machafuko na vitisho vya aina mbalimbali duniani.

Vilevile inatupasa kusema kuwa, mfumo wa kambi kadhaa peke yake hauwezi kudhamini amani na usalama wa dunia. Ukweli huu ulidhihirika barani Ulaya ambako licha ya mfumo wa kambi kadhaa kuwepo kwa kipindi cha karibu miaka mia moja lakini haukuandamana na utaratibu mzuri wa ushirikiano wa kimataifa na jinsi ya kutafuta ufumbuzi wa masuala mbalimbali; matokeo ya dosari hiyo yalikuwa kutokea Vita vya Kwanza vya Dunia.

Mtazamo huo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa unaungwa mkono na madola makubwa kama Russia na China ambazo hazikubaliani na sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani katika masuala ya kimataifa na zinasisitiza udharura wa kuwepo mfumo wa kambi kadhaa chini ya kivuli cha Umoja wa Mataifa. Mtazamo huu wa Russia na China kuhusu kuwepo kambi kadhaa duniani katika masuala ya kisiasa na kiuchumi hauifurahishi Marekani na kwa msingi huo serikali ya Washington hususan katika kipindi cha utawala wa Donald Trump inafanya kila liwezekanalo kukabiliana na mfumo huo.

 

Tags

Maoni