Feb 13, 2019 03:08 UTC
  • Russia: Iran ina haki ya kuimarisha teknolojia yake ya makombora

Serikali ya Russia imesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran in haki ya kuimarisha teknolojia yake ya makombora.

Katika mahojiano na shirika la habari la Sputnik hapo jana, Vladimir Ermakov, Mkurugenzi wa Idara ya Kudhibiti Silaha na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesisitiza kuwa, nyaraka za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa haziikatazi Iran kuunda, kuzalisha, kuzindua na kufanyia majaribio makombora yake ya balestiki, au hata kutuma satalaiti katika anga za mbali.

Kabla ya hapo, Segei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesisitiza kuwa Iran ina haki ya kujilinda, na mpango wake wa makombora haukiuki sheria za kimataifa.

Kuzinduliwa kombora la Fathul Mubin la Iran

Kadhalika Ofisi ya Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya nayo pia imetangaza kuwa, majaribio ya makombora yanayofanywa na Iran hayakiuki makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Katika miezi ya karibuni, serikali ya Marekani imedai mara kadhaa kwamba, shughuli za anga za mbali na za makombora ya Iran zinakiuka azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Tags

Maoni