Feb 15, 2019 02:52 UTC
  • Viongozi wa Russia, Iran na Uturuki watoa taarifa mwishoni mwa kikao chao cha mjini Sochi

Viongozi wa nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki wamesisitiza kuhusu azma yao ya kuimarisha ushirikiano kwa ajili ya kupeleka mbele gurudumu la mchakato wa kisiasa nchini Syria, kurejeshwa makwao wakimbizi na kuijenga upya nchi hiyo.

Marais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Vladimir Putin wa Russia na Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki wamesisitiza kupitia taarifa ya mwisho wa kikao chao cha nne cha kujadili kadhia ya Syria kilichofanyika jana mjini Sochi, Russia kwamba, wanaendelea kufungamana na kutilia mkazo mamlaka ya kujitawala, uhuru na kuheshimiwa umoja wa ardhi yote ya Syria kwa mujibu wa misingi ya hati ya Umoja wa Mataifa.

Taarifa hiyo imeashiria hali inavyoendelea hivi sasa kwenye medani za vita nchini Syria hasa baada ya kikao cha Septemba mwaka jana kilichofanyika hapa mjini Tehran na kueleza kwamba Iran, Russia na Uturuki zinatilia mkazo azma thabiti ziliyonayo ya kuanzisha haraka iwezekanavyo kamati ya katiba kupitia makubaliano juu ya muundo wake pamoja na ushauri na mapendekezo mbali mbali yaliyotolewa kuhusu uandaaji wa taratibu za kazi za kamati hiyo.

Kutoka kushoto: Rais Hassan Rouhani wa Iran, Rais Vladimir Putin wa Russia na Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki

Taarifa ya marais wa Iran, Russia na Uturuki imezungumzia pia umuhimu wa kuwepo uratibu na mashauriano kati ya pande husika katika mazungumzo ya amani ya Syria na Geir Pedersen, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya nchi hiyo.

Kwa mara nyingine tena viongozi wa nchi hizo tatu wameeleza bayana kuwa, mgogoro wa Syria hauwezi kutatuliwa kwa nguvu za kijeshi na mtutu wa bunduki na kwamba njia pekee ya kuuhitimisha mgogoro huo ni mchakato wa mazungumzo ya kisiasa baina ya Wasyria wenyewe kwa mujibu wa azimio nambari 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.../

Tags

Maoni