Feb 17, 2019 08:02 UTC
  • Vikwazo vipya; kuendelea njama za Marekani za kuzidisha mashinikizo dhidi ya Venezuela

Mgogoro wa Venezuela bado unaendelea ambapo Marekani na washirika wake wanatumia kila njia kwa ajili ya kuiondoa madarakani serikali halali ya mrengo wa kushoto ya Rais Nicolás Maduro na kuiweka pahala pake serikali kibaraka.

Katika mwendelezo wa mashinikizo ya Washington dhidi ya Rais Maduro, Wizara ya Fedha ya Marekani imewawekea vikwazo vipya vya kifedha shakhsia watano wa karibu na rais huyo wa Venezuela. Kwa mujibu wa vikwazo hivyo, fedha za watu hao zilizo nchini Marekani zitazuiliwa, sambamba na kuwazuia raia na mashirika ya Marekani kuamiliana nao. Vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Venezuela vimewekwa katika hali ambayo katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Washington ilianzisha mashinikizo kwa ajili ya kuing'oa madarakani serikali ya mrengo wa kushoto ya Rais Nicolás Maduro. Uungaji mkono wa Rais Donald Trump kwa Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani aliyejitangaza kuwa rais wa muda wa nchi hiyo, kushadidisha vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi na kadhalika vitisho vya kijeshi, ni miongoni mwa vita vya Marekani vinavyotumika kumshinikiza Rais Maduro aondoke madarakani. Katika uwanja huo mtandao mmoja wa habari nchini Lebanon umemnukuu Raymond Michael akisema: "Hii leo Washington inafanya njama kuhakikisha inadhibiti kikamilifu utajiri na msingi wa maamuzi ya nchi ya Simón Bolívar. Hususan kwamba tangu mwaka 2010 Marekani imekuwa na ndoto ya kutaka kudhibiti utajiri na vyanzo vya mafuta ya Venezuela." Mwisho wa kunukuu.

Jeshi la Venezuela ambalo linaendelea kuwa pamoja na Rais Nicolás Maduro 

Katika siku kadhaa zilizopita, viongozi wa Marekani wamekuwa wakitangaza uungaji mkono wao kwa matakwa ya Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani mwenye mfungamano na Washington ambapo katika uwanja huo wametuma katika mpaka wa Venezuela, shehena za chakula, madawa na misaada mingine ya kibinaadamu. Hatua ya serikali ya Venezuela ya kutoruhusu kuingia nchini humo shehena hizo za misaada, inatumiwa na Marekani na Wamagharibi kama wenzo wa kushadidisha upinzani wao dhidi ya serikali ya Rais Maduro sambamba na kupiga ngoma ya vita dhidi ya Venezuela. Guaidó anaamini kwamba, misaada hiyo ambayo inayotajwa kuwa ya kibinaadamu ya Marekani, inaweza kusadia kupunguza kwa kiasi fulani mgogoro wa chakula na madawa unaoikabili Venezuela kwa sasa. Hii ni katika hali ambayo mgogoro wa sasa wa kiuchumi nchini humo unatokana na siasa na uingiliaji wa Marekani na Wamagharibi ndani ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini. "Hivi karibuni Rais Nicolás Maduro akihutubu mjini Ciudad Bolívar aliitja misaada ya Marekani ambayo imetolewa kwa anwani ya misaada ya kibinaadamu kuwa ni chakula kichafu. Amesisitiza kwamba wanatuma misaada michafu ya chakula na kuanzisha propaganda katika hali ambayo sababu ya kupungua kwa mahitaji hayo muhimu nchini ni vikwazo vya Marekani."

Misaada ya Marekani kwa ajili ya kuwarubuni raia wa Venezuela ikielekea nchi hiyo

Ripoti za kiuchumi zinaonyesha kwamba, hasara iliyosababishwa na vikwazo vya Marekani dhidi ya Venezuela inafikia kiasi cha Dola bilioni 30 kwa mwaka. Aidha vikwazo vya mafuta vya Marekani dhidi ya nchi hiyo, vinatajwa kuwa vitakavyoikosesha serikali ya Caracas pato la kiasi cha Dola bilioni 11 kwenye sekta hiyo. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Rais Maduro akaitaja misaada hiyo ya Washington kwa nchi yake kuwa ni wenzo wa kuficha jinai za Marekani dhidi ya watu wa Venezuela na kusisitiza kwamba kabla ya hapo pia misaada kama hiyo ya Marekani kwenda kwa Afghanistan, Iraq, Syria na Libya, ilipelekea kusambaratishwa nchi hizo. Pamoja na hayo Juan Guaidó, kiongozi wa upinzani wa Venezuala bado ana matumaini kwamba kuingia misaada hiyo kutaandaa mazingira ya kuzidisha mapambano dhidi ya Rais Maduro. Hata hivyo licha ya juhudi zote za Washington na washirika wake dhidi ya serikali halali ya Caracas, bado kunaendelea kushuhudiwa umoja na mshikamano kati ya raia na askari wa nchi hiyo kwa maslahi ya rais huyo, kama ambavyo wameendelea pia kufungamana na matukufu ya mapinduzi ya Bolívar, suala ambalo limeizuia Washington kuweza kufikia malengo yake machafu nchini Venezuela. Pamoja na hayo bado mpambano wa kisiasa kati ya Marekani na Venezuela unaendelea.

Tags

Maoni