Mar 18, 2019 11:54 UTC
  • Kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) nchini Uturuki

Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan jana Jumapili alisema kuwa kikao cha dharura cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kitafanyika mjini Istanbul huko Uturuki.

Shah Mehmood Qureshi amesema kuwa, kikao hicho cha dharura cha Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa OIC kitafanyika tarehe 22 mwezi huu wa Machi kwa shabaha ya kuuunganisha Umma wa Kiislamu ili kukabiliana na propaganda chafu dhidi ya Uislamu, kuchukua hatua athirifu za kupambana na hujuma dhidi ya dini hiyo na kuchunguza athari mbaya za hujuma hiyo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan ameongeza kuwa, uamuzi huo umechukuliwa baada ya kufanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Uturuki, Mevlüt Çavuşoğlu.

Uamuzi wa kuitishwa kikao cha dharura cha nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) umechukuliwa siku chache baada ya magaidi wenye chuki dhidi ya Uislamu kushambulia misikiti miwili ya Linwood na Al-Noor katika mji wa Christchurch nchini New Zealand na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakiswali Swala ya Ijumaa. Katika hujuma hiyo ya kinyama Waislamu wasiopungua 52 waliuawa na wengine 47 wamejeruhiwa. Gaidi mwenye umri wa miaka 28 kwa jina Brenton Tarrant raia wa Australia mwenye asili ya Uingereza ndiye aliyyefanya shambulizi dhidi ya msikiti mmoja kati ya miwili iliyoshambuliwa nchini New Zealand. Awali gaidi huyo alikuwa akitangaza chuki na hasira zake katika mitandao ya kijamii dhidi ya wahajiri wa Kiislamu katika nchi za Ulaya.

Ukweli ni kwamba, katika mazingira ya sasa ya dunia kuna udharura mkubwa kwa nchi za Waislamu kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na wimbi la chuki na hujuma inayolenga Uislamu na matukufu yake hususan katika nchi za Magharibi. 

Hii ni kwa sababu katika upande mmoja kuongezeka idadi ya wahajiri Waislamu kutokana na machafuko na ukosefu wa amani katika nchi za Syria, Iraq na Afghanistan kumeibua jamii kubwa ya watu wanaohitajia himaya na msaada wa nchi na madola ya Kiislamu. 

Kwa upande mwingine wimbi kubwa la mashambulizi na hujuma dhidi ya Uislamu vinavyohochewa na propaganda chafu za mirengo na makundi yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia na mashambulizi ya kigaidi yanayowalenga Waislamu vimezidisha maradufu udharura wa kupewa himaya na kulindwa jamii za Waislamu.

Pamoja na hayo inatupasa kusisitiza kuwa, mashambulizi na hujuma dhidi ya Uislamu na taahira zake mbaya haviishii katika jamii za wahajiri wa Kiislamu tu bali wimbi hilo linaweza kuwa na taathira katika maamuzi yanayochukuliwa na viongozi serikali na tawala nchi za Magharibi kuhusiana na chi za Kiislamu.

HA Hellye ambaye ni mchambuzi katika Baraza la Atlantic anaamini kuwa: Hujuma na wimbi la propaganda chafu dhidi ya Uislamu havipaswi kupuuzwa kwa sababu kila mara kunapofanyika hujuma za aina hii huacha taathira hasi katika fikra za watu kuhusiana na Waislamu.

Kwa utaratibu huo kuna udharura kwa nchi za Kiislamu kutumia kwanza njia za kisiasa na kidiplomasia kwa ajili ya kuzishinikiza nchi za Magharibi zikomeshe wimbi la hujuma na propaganda chafu dhidi ya Uislamu na Waislamu. Nchi za Magharibi zinapaswa kulazimishwa kusitisha hujuma na propaganda chafu zinazochochea uhasama na chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu zinazoenezwa katika maeneo mbalimbali ya dunia kupitia jumbe za vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa kisingizio cha uhuru wa kusema na kujieleza.

Wakati huo huo nchi za Kiislamu zinalazimika kuchukua hatua madhubuti za kuwalinda na kuwatetea Waislamu wanaopatwa na madhara makubwa ya hujuma za wimbi la propaganda chafu dhidi ya dini yao na kufungua milango ya nchi hizo kwa ajili ya kupokea wahajiri wanaokimbia vita na mabalaa mengine na kuamiliana nao kwa mwenendo wa kibinadamu na Kiislamu.

Maoni