Mar 19, 2019 11:29 UTC
  • Radiamali kali ya Rais Macron dhidi ya harakati ya vizibao vya njano; kupigwa marufuku maandamano

Serikali ya Ufaransa imetangaza kupiga marufuku kufanyika maandamano au mkusanyiko wowote katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Marufuku hiyo inajumuisha kutofanyika maandamano katika mitaa ya Champs Elysees (Chanze Lize) katika mji mkuu Paris na katika miji mingine miwili ya Ufaransa. Serikali ya Ufaransa imechukua uamuzi huo ili kuhitimisha maadamano ambayo yamekuwa yakifanyika nchini humo ya harakati ya vizibao vya njano. 

Harakati ya vizibao vya njano iliyoanza nchini Ufaransa tangu tarehe 17 Novemba mwaka jana katika miji mbalimbali ya nchi hiyo ya bara Ulaya hususan mji mkuu Paris kwa minajili ya kulalamikia siasa na hatua za serikali ya Rais Emmanuel Macron imeendelea kuwa changamoto kuu kwa Rais Macron. Jumamosi iliyopita, maandamano ya vizibao vya njano nchini Ufaransa yalishuhudia machafuko na mapigano ambayo takribani hayakutarajiwa. Vurugu hizo zilitokea katika mitaa ya Champs Elysees (Chanze Lize) ambapo polisi waliwatia mbaroni zaidi ya watu 200.

Rais Emmanuel Macron

Maandamano ya wiki hii ambayo yalipewa jina la "Jumamosi Nyeusi" kinyume na matarajio ya maafisa wa serikali ya Ufaransa ambao walidhani idadi ya waandamanaji ingepungua, miji mbalimbali ya nchi hiyo ukiwemo mji mkuu Paris ilishuhudiwa wimbi kubwa la waandamanaji. Maandamano hayo ya Jumamosi yametajwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kutokea tangu lilipoibuka wimbi la maandamano ya vizibao vya njano nchini Ufaransa.

Maandamano ya vizibao vya njano ambayo awali yalianza nchini Ufaransa kwa ajili ya kupinga siasa za kiuchumi za Rais Emmanuel Macron hususan kuongezwa kodi ya mafuta ya dizeli, hadi sasa yamepelekea watu 11 kuuawa, zaidi ya 2000 kujeruhiwa huku waandamanaji wengine 8400 wakitiwa mbaroni. Aidha waandamanaji 1796 wamehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kuzusha vurugu na machafuko. Kadhalika watu wapatao 20 wamepoteza macho yao na kuwa vipofu kutokana na kushambuliwa kwa risasi za Flash-ball. 

Maandamano ya vizibao vya njano nchini Ufaransa

Matamshi yanayotolewa na viongozi wa Ufaransa ya kuichukulia hatua kali zaidi harakati ya vizibao vya njano, yamezitia wasiwasi mno asasi na makundi ya kutetea haki za binadamu nchini humo.

Mwezi uliopita pia, jumuiya hizo ziliashiria kuendelea malalamiko na maandamano ya vizibao vya njano na mkono wa chuma wa kikosi cha kuutuliza ghasia dhidi yya raia na kuelezea wasiwasi mkubwa zilizonao kuhusiana na kununuliwa silaha mpya na za mauaji za polisi zikiwemo silaha 1280 za Flash-ball.

Kwa kuzingatia upinzani mkali wa vizibao vya njano dhidi ya ahadi za Rais Macron,  inaonekana kuwa, Ikulu ya Elysee si tu kwamba,  haiko tayari kulegeza zaidi kamba, bali tunapaswa kutarajia ukandamizaji zaidi dhidi ya waandamanaji katika siku za usoni. Kwa hakika kuendelea maandamano ya vizibao vya njano kumezidi kuifanya serikali ya Rais Macron ikabiliwe na matatizo chungu nzima yakiwemo ya kiuchumi.

Polisi nchini Ufaransa wakiwa tayari kukabiliana na waandamanaji wa vizibao vya njano

Kuendelea maandamano ya vizibao vya njano nchini Ufaransa  kunaonyesha kuwa, harakati hii ya kijamii siyo malalamiko ya muda na ya mpito, bali ni tukio la kisiasa na kijamii na la kudumu lenye taathira kwa nchi hiyo ya Ulaya. Wakati huo huo, kudumu kwa harakati hii ambapo imepita miezi minne sasa tangu ilipoanza, kumekuwa na taathira yenye wigo mpana kwa mazingira ya ndani ya Ufaransa na hali ya uchumi ya nchi hiyo na hivyo kugeuka na kuwa daghadagha na hangaiko kuu la Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo.

Tajiriba ya miezi kadhaa iliyopita ya kuongezeka matakwa ya waandamanaji nchini Ufaransa kutoka madai ya kufutwa sheria ya ushuru na kuwa takwa la kuondoka madarakani Rais Macron imeonyesha kuwa, kuchukua hatua kali na za ukandamizaji dhidi ya wapinzani, si tu kwamba, hakutaifanya azma na irada ya harakati ya vizibao vya njano idhoofike katika kufuatilia matakwa yake, bali ukandamizaji huo umewafanya waandamanaji wa harakati hiyo wawe na misimamo mikali zaidi.

Maoni