Mar 19, 2019 15:04 UTC
  • 'Uenezaji chuki dhidi ya Waislamu, sababu kuu ya mashambulizi ya kigaidi New Zealand'

Mamia ya wanachuoni na viongozi wakubwa wa Kiislamu kutoka kona zote za dunia wamesema kuwa, kampeni ya kueneza chuki dhidi ya Uislamu ndiyo sababu kuu ya kutokea mauaji ya kikatili na ya umati dhidi ya Waislamu waliokuwa wanafanya ibada katika misikiti miwili ya mjini Christchurch nchini New Zealand.

Kwa uchache gaidi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Brenton Tarrant aliwapiga risasi na kuwaua shahidi Waislamu 50 na kuwajeruhi wengine 50, tisa kati yao wakiwa katika hali mahututi, wakati Waislamu hao walipokuwa kwenye misikiti hiyo miwili kwa ajili ya Sala ya Ijumaa.

Gaidi huyo raia wa Australia mwenye asili ya Uingereza alikuwa anarusha hewani mubashara kwenye Facebook video iliyokuwa inaonesha moja kwa moja jinai yake hiyo. Gaidi huyo ambaye alisema katika maneno yake marefu ya maandishi kwamba ameathiriwa na misimamo ya rais wa Marekani, Donald Trump, aliwaita Waislamu wanaoishi barani Ulaya kuwa ni wavamizi wanaostahiki kuuawa.

Gaidi Brenton Tarrant aliyefanya mauaji ya kutisha dhidi ya Waislamu nchini New Zealand

 

Vile vile gaidi huyo aliandika: "Tunakuja Constantinople (yaani Istanbul Uturuki) na tutaangamiza kila msikiti na mnara (wa msikiti) katika mji huo. Maeneo ya Hagia na Sophia yatakombolewa kutokana na minara ya misikiti, Constantinople (Istanbul) itakuwa tena katika mikono inayostahiki; ya Wakristo."

Zaidi ya viongozi 350 wakubwa wa Kiislamu kutoka kona zote za duniani zikiwemo Uingereza, Marekani na Afrika Kusini jana Jumatatu walitia saini barua waliyoituma kwa gazeti la The Guardian la Uingereza wakilaani jinsi vyombo vya habari vya Magharibi pamoja na wanasiasa, wasomi na watu wa vitengo vya kielimu huko Ulaya na Marekani wanavyoeneza chuki dhidi ya Uislamu na kusisitiza kuwa, hilo ndilo lililopelekea kutokea maafa kama hayo ya New Zealand dhidi ya Waislamu wasio na hatia.

Maoni