Mar 19, 2019 15:54 UTC
  • CNN yatoa indhari: Uzima wa kiakili wa Trump unazidi kupungua siku baada ya siku

Kanali ya televisheni ya CNN ya Marekani imetahadharisha kuwa afya ya rais wa nchi hiyo Donald Trump kwa upande wa akili inazidi kuwa mbaya siku baada ya siku.

Kanali hiyo ya televisheni ya Marekani imetoa indhari hiyo kutokana na ripoti za wataalamu wa maradhi ya akili.

CNN imemnukuu George Conway, mume wa Kelyanne Conway, mshauri mwandamizi wa rais Donald Trump wa Marekani na mkurugenzi wa zamani wa timu ya kampeni ya kiongozi huyo, aliyeandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba: Hali ya kiakili ya Trump inaanza kuwa mbaya, hivyo Wamarekani wote wanapaswa kulitafakari suala hilo kwa uzito mkubwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika ujumbe wake wa Twitter, George Conway ameashiria ripoti kuhusu matatizo ya kisaikolojia na kiakili na kueleza kwamba, Trump ana matatizo ya kinafsi ya kujigamba na kujikweza na kusumbuliwa na hali ya kutopenda kuchanganyika kijamii. Hata hivyo Bi Kelyanne Conway amesema, haafikiani na maelezo ya mumewe.

Dokta Lise Van Susteren, mtaalamu wa maradhi ya kisaikolojia nchini Marekani ameieleza kanali ya televisheni ya CNN kuwa, yeye hajawahi kumkagua kiafya Trump, lakini kutokana na alivyomuona kwenye televisheni amefikia hitimisho kwamba anayo matatizo ya kinafsi na kishakhsia yaliyotajwa.

Hadi sasa taasisi kadhaa za taaluma ya saikolojia nchini Marekani zimeonya na kutahadharisha kuhusu hali ya Trump ya kutokuwa na uzima kamili wa kiakili na kinafsi na kutangaza kwamba kiongozi huyo hana uzima kamili wa kisaikolojia na kitabia unaotakiwa kwa ajili ya kutekeleza majukumu na masuulia ya urais wa nchi hiyo.../

Maoni