Mar 20, 2019 16:13 UTC
  • Russia: Marekani isijaribu kuingilia kijeshi Venezuela, tutahakikisha tunalinda maslahi yetu

Serikali ya Russia imeionya vikali Marekani isijaribu kufanya uingiliaji wa aina yoyote wa kijeshi nchini Venezuela na kusisitiza kwamba Moscow italinda maslahi yake nchini humo.

Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameyasema hayo alipokutana na mwakilishi maalumu wa Marekani katika masuala ya Venezuela, ambapo akiashiria tofauti kuu zilizopo kati ya Washington na Moscow katika masuala ya Venezuela, ameitahadharisha Marekani isijaribu kutumia chaguo la kijeshi dhidi ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia

Ryabkov amesisitiza kwamba Russia inapinga vikali njama zozote za Marekani za kutumia misaada ya kibinaadamu kwa ajili ya kuingilia masuala ya ndani ya Venezuela na katika hilo imeendelea kusisitiza kwamba misaada yoyote kwa ajili ya nchi hiyo ni lazima itolewe kwa kupitia njia ya ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na si vinginevyo. Kadhalika Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa, maslahi ya Russia nchini Venezuela ni lazima yalindwe na kwamba Moscow inazidi kupatwa na wasi wasi kila siku kutokana na vikwazo vya Marekani dhidi ya nchi hiyo. Jumanne ya jana Rais Donald Trump wa Marekani alinukuliwa akisema kuwa, machaguo yote kwa ajili ya Venezuela yako mezani.

Tags

Maoni