Mar 21, 2019 03:51 UTC
  • Kiongozi wa ngazi ya juu Kashmir ya Pakistan aionya Israel kwa kuingilia masuala ya eneo hilo

Kiongozi mkuu wa eneo la Kashmir ya upande wa Pakistan ameuonya utawala haramu wa Kizayuni Israel kutokana na uingiliaji wake katika masuala ya eneo hilo.

Masood Khan ametoa onyo hilo akizungumzia uingiliaji wa utawala wa Kizayuni katika mzozo wa hivi karibuni kati ya India na Pakistan na kueleza kuwa uwepo wa Wazayuni katika eneo utasababisha kushtadi mizozo ya eneo la kusini mwa Asia. Kiongozi mkuu wa eneo la Kashmir ya Pakistan amesisitiza kwamba, kutatuliwa mzozo wa Kashmir kutaondosha tofauti zilizopo za katika eneo na kwa ajili hiyo amezitaka serikali za Islamabad na New Delhi zitumie njia ya udiplomasia kwa ajili ya kumaliza mvutano baina yao. Hii sio mara ya kwanza ambapo serikali ya Pakistan inailaumu vikali Israel kwa kuhusika katika kuchochea mzozo ndani ya eneo hilo kwa maslahi ya India.

Masood Khan

Inafaa kuashiria kuwa, sehemu moja ya Kashmir ipo upande wa India huku nyingine ikiwa upande wa Pakistan, ambapo hata hivyo pande zote mbili zimekuwa zikidai umiliki wa Kashmir yote. Duru mpya ya mzozo kati ya India na Pakistan, iliibuka baada ya shambulizi la kigaidi lililotekelezwa Februari 14 mwaka huu katika eneo la Kashmir ya upande wa India ambapo kwa akali watu 44 waliuawa huku kundi la kigaidi la Jaish-e-Mohammed likinyooshewa kidole cha tuhuma za kuhusika na hujuma hiyo. Baada ya shambulizi hilo, ndege za kivita za India zilifanya mashambulizi makali katika maeneo yaliyodaiwa kuwa ngome za magaidi ndani ya Pakistan. Kwa mujibu wa India watu 300 wapatao waliuawa, lakini Pakistan ilikanusha madai hayo.

Baadhi ya duru za habari zimeripoti kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ulishiriki kwenye mashambulio ya anga ya India ndani ya ardhi ya Pakistan.

Maoni