Mar 21, 2019 15:04 UTC
  • Misikiti mitano yavamiwa katika mji wa Birmingham nchini Uingereza

Misikiti mitano imeshambuliwa katika mji wa Birmingham nchini Uingereza, wiki moja baada ya kutokea mashambulizi ya kigaidi nchini New Zealand na kuua makumi ya Waislamu na kujeruhi makumi ya wengine.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Sajid Javid amesema kushambuliwa misikiti mitano katika mji wa Birmingham ulioko katikati mwa nchi ni jambo la kutia wasiwasi na kwamba mienendo hiyo ya chuki na ubaguzi ni kitu kisichokuwa na nafasi na kisichokubalika katika jamii ya nchi hiyo.

Habari zinasema kuwa, madirisha ya misikiti hiyo yamevunjwa kwa kutumia nyundo. Kituo cha Kiislamu cha Barabara ya Witton pia kilishambuliwa usiku wa kuamkia leo na mtu aliyeripotiwa kuwa na nyundo. 

Msikiti wa Jamia wa Ghousia katika Barabara ya Albert katika eneo la Aston mjini Birmingham ni miongoni mwa misikiti hiyo mitano iliyoshambuliwa usiku wa kuamkia leo.

 

Maandamano London ya kulaani mauaji ya kigaidi ya Waislamu wa New Zealand

Kamanda Mkuu wa Polisi katika eneo la West Midlands, Dave Thompson amesema chanzo cha hujuma hizo za jana usiku hakijajulikana, lakini maafisa wa Kitengo cha Kupambana na Ugaidi wanachunguza matukio hayo.

Katika kipindi cha chini ya masaa 24 tangu magaidi kufanya jinai kubwa na ya kutisha dhidi ya Waislamu nchini New Zealand, magaidi wengine waliuvamia msikiti mmoja mjini London na kumjeruhi kijana mmoja wa Kiislamu, mbali na kuwatukana kwa sauti kubwa Waislamu na dini yao Jumamosi iliyopita.

 

Tags

Maoni